Kocha mpya Cameroon awatema Onana, Vincent Aboubakar
Muktasari:
- Onana anayekipiga Trabzonspor ya Uturuki kwa mkopo akitokea Manchester United ya England, ni miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu walioachwa kwenye kikosi cha Cameroon sambamba na mshambuliaji Vincent Aboubakar, ambaye amekuwa mhimili kwenye kikosi cha timu hiyo kwa zaidi ya miaka 15.
Kipa Andre Onana ameachwa kwenye orodha ya wachezaji wanaounda kikosi cha Cameroon kitakachoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zitakazoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco, huku David Pagou akitajwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua nafasi ya Mbelgiji, Marc Brys.
Onana anayekipiga Trabzonspor ya Uturuki kwa mkopo akitokea Manchester United ya England, ni miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu walioachwa kwenye kikosi cha Cameroon sambamba na mshambuliaji Vincent Aboubakar, ambaye amekuwa mhimili kwenye kikosi cha timu hiyo kwa zaidi ya miaka 15.
Mabadiliko hayo yamekuja baada ya Cameroon kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika nchini Mexico, Canada na Marekani.
Kiungo mshambuliaji wa Manchester United, Bryan Mbeumo, amejumuishwa kwenye kikosi hicho, pamoja na kiungo wa Brighton & Hove Albion, Carlos Baleba.
Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon, Samuel Eto’o, hakuwahi kuficha nia yake ya kumwondoa kocha Brys tangu alipoteuliwa na Wizara ya Michezo mwezi Aprili 2024, na amewahi kujaribu kufanya hivyo mara kadhaa hapo awali.
Baada ya wiki iliyopita kuchaguliwa tena kuwa Rais Shirikisho la Soka Cameroon, Eto’o amechukua hatua nyingine na kumwondoa Mbelgiji huyo, kisha kumteua Pagou, mwenye umri wa miaka 56, ambaye amewahi kufundisha timu kadhaa katika ligi ya ndani ya Cameroon na atasaidiwa na Martin Ntoungou Mpile.
Katika AFCON 2025, Cameroon itaanza kampeni yao ya Kundi F dhidi ya Gabon jijini Agadir mnamo Desemba 24, 2025. Pia wako kwenye kundi moja na mabingwa watetezi Ivory Coast pamoja na Msumbiji.
Kikosi cha Cameroon
Makipa: Devis Epassy (Dinamo Bucharest), Simon Omossola (St Eloi Lupopo), Simon Ngapandouetnbu (Montpellier) na Edouard Sombang (Colombe Du Dja).
Mabeki: Samuel Kotto (Gent), Gerzino Nyamsi (Lokomotiv Moscow), Jean-Charles Castelletto (Al-Duhail), Nouhou Tolo (Seattle Sounders), Flavien Enzo Boyomo (Osasuna), Mahamadou Nagida (Rennes), Christopher Wooh (Spartak Moscow), Junior Tchamadeu (Stoke City) na Darlin Yongwa (FC Lorient).
Viungo: Martin Ndzie (Rapid Vienna), Carlos Baleba (Brighton & Hove Albion), Arthur Avom (FC Lorient), Eric-Junior Dina Ebimbe (Brest), Brice Ambina (Valerenga), Jean Junior Onana (Genoa) na Olivier Kemen (Istanbul BB).
Washambuliaji: Bryan Mbeumo (Manchester United), Christian Bassogog (Al-Okhdood), George-Kevin N’Koudou (Al-Diriyah), Danny Namaso (Auxerre), Frank Magri (Toulouse), Karl Etta Eyong (Levante), Christian Kofane (Bayer Leverkusen) na Patrick Soko (Almeria).