Asamoah Gyan amtaja bingwa AFCON 2025
Muktasari:
- Asamoah ambaye aliitumikia Ghana katika mechi 109 na kufunga mabao 51, amesema anaamini Nigeria, Ivory Coast na Morocco, ni mataifa ambayo yana nafasi kubwa ya kuibuka na ubingwa wa AFCON 2025.
Kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), mwanasoka wa zamani wa timu ya Taifa ya Ghana, Asamoah Gyan, ametaja nchi tatu ambazo anaamini huenda mojawapo ikatwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Gwiji huyo amezitaja nchi hizo akiwa katika hafla ya utoaji tuzo za CAF nchini Morocco, jana Jumatano, Novemba 19, 2025.
Asamoah ambaye aliitumikia Ghana katika mechi 109 na kufunga mabao 51, amesema anaamini Nigeria, Ivory Coast na Morocco, ni mataifa ambayo yana nafasi kubwa ya kuibuka na ubingwa wa AFCON 2025.
Amesema anaamini ushindani utakuwa mkubwa kwenye michuano hiyo, lakini bado anaziona nchi hizo tatu kuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi, kutokana na kuwa na vikosi bora na imara ambavyo vinaweza kupambana kwa mbinu tofauti na kupata matokeo mazuri.
“Tuna timu nyingine zinakwenda kushiriki fainali za AFCON 2025, nafahamu Ghana haipo mwenye michuano hii lakini tumefuzu Kombe la Dunia. Kwangu ninaona Nigeria, Ivory Coast na Morocco zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kutwaa ubingwa wa AFCON 2025.
“Nigeria ilifanya vizuri katika michuano ya AFCON iliyopita, ilikaribia kutwaa ubingwa, lakini ilipoteza dhidi ya waliokuwa wenyeji Ivory Coast, ambayo pia bado ninaiona ina nafasi nzuri ya kuendelea kufanya maajabu katika michuano hiyo ya Afrika.
“Kwa upande wa Morocco ni timu yenye nguvu, ambayo pia inafanya vizuri kwa sasa. Kwa hiyo nchi hizi tatu sina kipingamizi nazo kabisa, ninaamini moja kati ya hizi zitaibuka bingwa wa AFCON 2025,” amesema Asamoh.
Timu ya taifa ya Morocco imefuzu moja kwa moja AFCON 2025 kwa kuwa nchi mwenyeji wa michuano hiyo, hivyo haikuhesabiwa katika zilizopitia mchujo.
Hata hivyo, ilicheza mechi za mchujo dhidi ya Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Lesotho, na ilimaliza kinara wa kundi hilo. Hii ilionyesha kuwa Morocco si tu mwenyeji, bali pia timu yenye nguvu na imejiandaa vyema kushindana katika kombe la mataifa ya Afrika.
Kwa upande wa Nigeria, imefuzu AFCON 2025 kupitia hatua ya mchujo baada ya kuongoza Kundi D, ambapo safari ya kufuzu iliimarishwa zaidi baada ya Libya kupata ushindi wa 1–0 dhidi ya Rwanda, matokeo yaliyoipa Nigeria nafasi ya mapema ya kufuzu.
Katika moja ya mechi muhimu, Victor Osimhen alifunga bao la kusawazisha dhidi ya Benin, na alama hiyo ikawa muhimu katika kuendelea kwao. Zaidi ya hapo, CAF iliikabidhi Nigeria ushindi wa 3–0 dhidi ya Libya baada ya matatizo ya kiufundi yaliyosababisha mechi hiyo kushindwa kuchezwa.
Mfululizo wa matokeo haya uliifanya Nigeria kuongoza kundi lao, hivyo kupata tiketi ya AFCON 2025 bila changamoto kubwa.
Ivory Coast imefuzu AFCON 2025 kupitia mechi za mchujo wa Kundi G, ikicheza na kupata ushindi dhidi ya Zambia na Sierra Leone.
Katika mechi yao ya mwisho ya mchujo, Ivory Coast iliibuka na ushindi wa 4–0 dhidi ya Chad, na kujihakikisha nafasi yao kwenye fainali hizo.
Kwa matokeo hayo, Ivory Coast ilimaliza nafasi ya pili kwenye Kundi G na kupata tiketi ya kushiriki AFCON 2025.