Kocha Liverpool awaonya mastaa wake

Muktasari:
- Liverpool ambayo kwa sasa inaongoza ligi kwa tofauti ya alama 12, mbele ya Arsenal, imebakisha mechi tisa tu kabla ya kumaliza msimu huu.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amewatahadharisha wachezaji wake kwamba milele wataandamwa na kuimbwa ikiwa watashindwa kushinda taji la Ligi Kuu England msimu huu.
Liverpool ambayo kwa sasa inaongoza ligi kwa tofauti ya alama 12, mbele ya Arsenal, imebakisha mechi tisa tu kabla ya kumaliza msimu huu.
Lakini kiwango chao katika siku za hivi karibuni kuanzia fainali ya Carabao dhidi ya Newcastle United na hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa ambapo walitolewa na Paris Saint-Germain kimezua wasiwasi mkubwa kwa mashabiki wao.
Slot anajua kuwa gharama ya kushindwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu itakuwa ni jambo la aibu sana kwao lakini anasisitiza yeye ni kocha ambaye kila wakati atachukulia anguko kama sehemu ya kujifunza.
“Najua jinsi inavyokuwa, ikiwa hutapata mataji kama kocha au mchezaji, inaweza kuwa jambo baya kwako,” alisema Slot kupitia kitabu chake cha safari yake ya ukocha.
“Kuna njia tofauti za kukumbukwa. Angalia timu ya Uholanzi katika Kombe la Dunia la 1974. Kila mtu aliona Kombe la Dunia kama mashindano ambayo Uholanzi wangepata chochote lakini hawakurudi nyumbani na kombe. Nataka kushinda michezo mingi iwezekanavyo, pia nataka kubaki katika kumbukumbu za watu.
“Napenda sana wakati watu wanaponielezea kama kocha ambaye kila wakati anafikiri kwa mtindo wa mashambulizi. Kadri unavyoshambulia, unaboresha nafasi zako za kushinda.”
Arsenal ndio tishio kubwa kwa matumaini ya Liverpool ya kushinda taji katika msimu wa kwanza wa Slot akiwa kocha wa timu hiyo baada ya kuchukua nafasi ya Jurgen Klopp.
Mchezo unaofuata, majogoo hawa watakutana na Everton, Aprili 2 katika dimba la Anfield.
Slot aliongoza Feyenoord kushinda taji la Ligi Kuu Uholanzi mwaka 2023.