Kocha Liverpool afichua udhaifu wa kikosi chake
Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ligi Kuu England walikwepa kukumbana na kipigo cha tano mfululizo, ambacho kingeandikisha mwanzo wa hovyo wa msimu katika kipindi cha miaka 73 baada ya kuichapa 5-1 Eintracht Frankfurt kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano iliyopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amefunguka udhaifu wa kikosi chake kinachofanya timu hiyo kutaabika kwenye baadhi ya mechi za msimu huu.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England walikwepa kukumbana na kipigo cha tano mfululizo, ambacho kingeandikisha mwanzo wa hovyo wa msimu katika kipindi cha miaka 73 baada ya kuichapa 5-1 Eintracht Frankfurt kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano iliyopita.
Kocha Slot alikiri kikosi chake cha Liverpool kilikuwa kwenye wakati mgumu wa kukabiliana na soka la mipira ya juu na pasi ndefu na hivyo kupoteza.
Frankfurt ilikuwa tofauti na mtindo wao wa uchezaji uliwafanya wakumbane na kipigo cha Liverpool. Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa Slot, kama unataka kuichapa Liverpool unahitaji kucheza soka la kupiga mipira mirefu kwenda mbele.
Na hilo linaweza kuwa ni habari njema kwa kocha wa Brentford, Keith Andrews, ambaye kikosi chake kitakabiliana na Liverpool, Jumamosi, kama watachagua kucheza soka la mipira mirefu, ambalo wamekuwa mahiri, wanaweza kuiadhibu timu hiyo ya Anfield.
Liverpool ilipoteza mechi dhidi ya Crystal Palace, Galatasaray, Chelsea na Manchester United kabla ya kwenda kuzinduka huko Ujerumani.
“Tofauti kubwa kwenye mechi hii kwa kulinganiahs na zile zilizopita ni staili ya uchezaji ya wapinzani wetu," amesema na kuongeza. “Katika mechi nne zilizopita tulishindwa kukabiliana na wapinzani ambao hawakuwa wakicheza soka la ardhini, wanacheza juu tu.”
Kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amesema anafurahi kuona timu za Ligi Kuu England zinabadili mara kwa mara staili ya uchezaji wa soka lao.