Kocha Genk amtuliza Samatta

KOCHA wa KRC Genk, Wouter Vrancken amewataka wachezaji wake kujitoa haswa kwenye mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Royal Antwerp bila kuzingatia matokeo ya mchezo mwingine wa mchujo kati ya Royale Union Saint-Gilloise dhidi ya Club Brugge kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji 'Jupiler Pro'.

Raundi ya mwisho kwenye mchujo wa ubingwa w Ligi Kuu Ubelgiji itachezwa kesho, Jumapili huku presha ikipanda na kushuka kwa mashabiki wa KRC Genk anayoichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, Royal Antwerp na Royale Union Saint-Gilloise ambazo zipo kwenye nafasi ya kwanza hadi tatu.

Vrancken alisema hayo ili wachezaji wake waelekeze fikra na mawazo yao kwenye mchezo wao dhidi ya Royal Antwerp,"Ni mbaya wakati unacheza kuwa na mawazo ya matokeo ya mchezo mwingine hiyo ni mbaya inaweza kupunguza ufanisi wao."

"Tunatakiwa kufanya vizuri kwanza halafu hayo  mambo mengine yatafuata baadae, tunataka kuwapa kilichobora mashabiki wetu ambao wamekuwa pamoja na sisi tangu mwanzoni mwa msimu," alisema kocha huyo ambaye enzi zake alikuwa kiungo mkata umeme.

Katika mchezo huo wa mwisho wa msimu, nahodha wa Taifa Stars, Samatta ndiye atakayekuwa na jukumu la kuongoza mashambulizi ya KRC Genk ambayo ipo nafasi ya tatu kwenye mchujo wa ubingwa ikiwa na pointi moja nyuma ya vinara, Royal Antwerp na Royale Union Saint-Gilloise wenye pointi 46.

Samatta na wenzake watakuwa wakisaka ushindi dhidi ya Royal Antwerp huku wakiombea mchezo kati ya Royale Union Saint-Gilloise ambao wapo juu yao wachapwe au kutoka sare dhidi ya bingwa mtetezi, Club Brugge.

Matokeo yakienda hivyo basi, Samatta atatwaa ubingwa wake wa pili wa Ligi Kuu Ubelgiji akiwa na KRC Genk, ikumbukwe ubingwa wake wa kwanza alitwaa msimu wa  2018–19 ambao alitupia mabao 23 kabla ya mchujo wa ubingwa.

Msimu huu ambao kwa Ubelgiji utatamatika kesho, Samatta ametupia mabao saba.