Kocha Chelsea aonya kuhusu Cole Palmer
Muktasari:
- SunSport ilifichua wiki hii kuwa Palmer angefikiria kuhamia Old Trafford kwa sababu anajihisi kutotulia jijini London.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Liam Rosenior ameonya kwamba Cole Palmer hagusiki kabisa Chelsea, licha ya hofu kubwa kuibuka kuwa yuko tayari kujiunga na Manchester United.
SunSport ilifichua wiki hii kuwa Palmer angefikiria kuhamia Old Trafford kwa sababu anajihisi kutotulia jijini London.
Hata hivyo, kocha mpya wa Chelsea, Rosenior, anasisitiza kuwa nyota huyo wa England mwenye umri wa miaka 23 ana furaha Stamford Bridge.
Palmer alisafiri kwenda Naples na kikosi cha Chelsea baada ya kukosa mechi mbili zilizopita kutokana na jeraha la paja.
Rosenior amesema: “Je, hagusiki? Je, ana furaha? Ndiyo na ndivyo.
“Ni rahisi sana, Cole Palmer ni mchezaji wa ajabu kama wachezaji wengine wengi kwenye kikosi. Cole yuko hapa, ana furaha sana na nasubiri kwa hamu kumwona tena uwanjani. Cole ana furaha kubwa. Nimekuwa na mazungumzo mengi naye.
“Mawazo yetu yapo kwenye jinsi tunavyoweza kuboresha timu hii, jinsi yeye anavyoweza kuimarika na jinsi ninavyoweza kusaidia. Anapenda kuwa hapa na anataka kuwa mchezaji wa Chelsea.”
Palmer alijiunga na Chelsea akitokea Manchester City kwa ada ya Pauni 42.5 milioni miaka mitatu iliyopita na ana mkataba hadi mwaka 2033.
Tangu hapo, ameichezea klabu hiyo mara 110, akifunga mabao 48 na kuasisti mara 28. Na amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha England akitumika katika mechi 12. Kwa sasa Chelsea ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuelekea mechi yao dhidi ya Napoli usiku wa Jumatano.
Ushindi utawafanya wafuzu moja kwa moja kwenda hatua ya 16 bora isipokuwa Barcelona au Sporting Lisbon washinde kwa tofauti ya mabao mawili zaidi.
Manchester City, Atletico Madrid na Atalanta pia zinaweza kuipita Chelsea, lakini watahitaji ushindi wa mabao mengi zaidi. Mechi zote zilichezwa usiku wa Jumatano.
TAKWIMU ZA PALMER KWENYE SOKA LAKE
2020/21: Man City; mechi 2, mabao 0, asisti 0
2021/22: Man City; mechi 11, mabao 3, asisti 1
2022/23: Man City; mechi 25, mabao 1, asisti 1
2023/24: Chelsea; mechi 45, mabao 25, asisti 15
2024/25: Chelsea; mechi 46, mabao 15, asisti 11
2025/26: Chelsea; mechi 19, mabao 8, asisti 2
2023-: England; mechi 12, mabao 2, asisti 1