Kocha Chelsea amjibu wakala wa Enzo
Muktasari:
- Fernandez, 25, aliondolewa kwenye kikosi kwa mechi mbili baada ya kutoa kauli zilizoonyesha dalili za kutaka kujiunga na Real Madrid kabla na wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Liam Rosenior ametoa majibu juu ya kauli ya wakala wa Enzo Fernandez, Javier Pastore, aliyedai adhabu aliyopewa mchezaji huyo “si ya haki kabisa.”
Fernandez, 25, aliondolewa kwenye kikosi kwa mechi mbili baada ya kutoa kauli zilizoonyesha dalili za kutaka kujiunga na Real Madrid kabla na wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Argentina alizungumzia wazi uwezekano wa kuishi jijini Madrid, huku pia akiwataja magwiji wa klabu hiyo Toni Kroos na Luka Modric ni miongoni mwa wachezaji anaowakubali sana na anatamani kufika katika levo zao.
Uongozi wa Chelsea uliamua kumfungia Enzo kucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Port Vale, pamoja na kukosa nechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City Jumapili ijayo.
Baada ya Chelsea kupata ushindi mkubwa wa mabao 7-0 na kufuzu nusu fainali , Rosenior aliulizwa kuhusu kauli za Pastore, akajibu: "Huo ni mtazamo wake. Sina la kusema kuhusu maoni ya mtu mwingine. Enzo anajua ninavyofikiria juu yake na ilikuwa vizuri kumwona leo akija kuwaunga mkono wachezaji wenzake akiwa jukwani. Tutasonga mbele na kuhakikisha tunamaliza msimu vizuri."
Rosenior pia aliulizwa kama Fernandez aliomba radhi kwa wachezaji wenzake, akasema:
"Nilisema jana, mazungumzo yangu na wachezaji wangu ni binafsi, iwe ni Enzo au mwingine yeyote, hubaki ndani ya timu. Chumba cha kubadilishia nguo ni sehemu takatifu. Nilieleza wazi ninavyomfahamu na ninavyomwangalia, ni kijana mzuri sana. Kwa sasa mimi na Enzo tuko kwenye uhusiano mzuri. Nilionana naye leo, tukazungumza vizuri ana kwa ana na mambo hayapo kama watu wanavyodhani."