Kimeumana Chelsea! Enzo Fernandez apigwa ‘pini’, Cucurella matatani
Muktasari:
- Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior amethibitisha Fernandez hatakuwa kwenye kikosi chake wakati wa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Port Vale kesho Jumamosi na mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester City wiki ijayo.
Chelsea imeingia katika kipindi cha misukosuko baada ya kiungo wake tegemeo, Enzo Fernandez kupewa adhabu kali kutokana na matamshi yake yaliyoashiria kutaka kuondoka klabuni hapo na kujiunga na miamba ya Uhispania, Real Madrid.
Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior amethibitisha Fernandez hatakuwa kwenye kikosi chake wakati wa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Port Vale kesho Jumamosi na mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester City wiki ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Ijumaa, Aprili 03, 2026 Rosenior amesema uamuzi huo umefikiwa kwa pamoja na uongozi wa klabu baada ya kubaini mchezaji huyo amevunja miiko na utamaduni wa timu hiyo ya jijini London.
“Tulizungumza na Enzo saa moja iliyopita. Kama klabu na mimi nikiwa sehemu ya mchakato huo, tumefanya maamuzi. Hatokuwa sehemu ya kikosi cha Chelsea kesho Jumamosi wala dhidi ya Manchester City,” amesema Rosenior na kuongeza:
“Inasikitisha kuona Enzo akizungumza vile. Binafsi sina neno baya dhidi ya tabia yake, lakini alivyunja utamaduni wa klabu hii na kile tunachotaka kujenga. Ilibidi tutoe adhabu.”
Hata hivyo, Rosenior amesisitiza kuwa mlango haujafungwa kabisa kwa kiungo huyo wa Argentina, akisema bado anamheshimu kwa mafanikio yake na anajua Enzo ana shauku ya kuona Chelsea ikifanikiwa.
Sakata la Fernandez liliibuka baada ya mchezaji huyo kuhoji mustakabali wake ndani ya Stamford Bridge baada ya kichapo dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG). Siku chache baadaye, akiwa kwenye mahojiano ya mubashara na chaneli ya SpiderCARP ya Argentina, Enzo alionekana kutamani kujiunga na Real Madrid.
Alipoulizwa ni jiji gani lingine angependa kuishi, Enzo alijibu: “Madrid... Naipenda sana Madrid... inafanana sana na Buenos Aires.” Kauli hiyo ilitafsiriwa kama ombi la kutaka kusajiliwa na mabingwa hao kihistoria Ulaya.
Mbali na Enzo, Kocha Rosenior alifanya kikao cha dharura na beki Marc Cucurella baada ya mchezaji huyo kukosoa hadharani mkakati wa usajili wa klabu na kufukuzwa kwa aliyekuwa kocha mkuu, Enzo Maresca.
Cucurella, katika mahojiano aliyofanyiwa wakati wa mapumziko ya kimataifa, alidai sera ya klabu ya kusajili wachezaji vijana pekee inakwamisha azma ya kutwaa mataji makubwa.
“Tulipoteza dhidi ya PSG kwa sababu tulikosa wachezaji wenye uzoefu wa mechi kama zile. Kusajili vijana pekee kunaweza kufanya malengo ya kutwaa makombe kuwa magumu,” alisema Cucurella.
Rosenior alieleza alikuwa na mazungumzo ya nusu saa ofisini kwake na Cucurella. Alimkumbusha mchezaji huyo anapaswa kueleza malalamiko yake ndani ya klabu badala ya kwenye vyombo vya habari.
“Nimesikitishwa na mahojiano ya Marc. Alipaswa kuzungumza nasi kwanza kuhusu hisia zake. Tunataka wachezaji wawe wawazi kwa faida ya klabu, kama alivyofanya Reece James ambaye sasa amesaini mkataba mpya kwa sababu anaamini katika mradi wetu,” amesema Rosenior.
Licha ya mvutano huo, kocha huyo amehakikisha Cucurella bado amejitolea kikamilifu kwa Chelsea na anaamini katika safari ya klabu hiyo kuelekea mafanikio.