Kauli ya Enzo Fernandez yaibua maswali Chelsea
Muktasari:
- Katika hilo, Telegraph imefichua kwamba baadhi ya nyota wa Chelsea hawafurahishwi na mwenendo wa mchezaji mwenzao, Enzo Fernandez, ambaye hivi karibuni alisema hajui nini hatma yake katika viunga vya Stamford Bridge baada ya kuhusishwa na Real Madrid.
LONDON, ENGLAND: PILIKAPILIKA za usajili wa dirisha kubwa la wachezaji zimeshaanza kupamba moto huko Ulaya, ambako mastaa kibao wamekuwa wakihusishwa kubadili klabu, na wengine kulamba dili tamu msimu ujao. Na hivyo ndivyo kwa kila staa mkubwa Ulaya kuanza kuhusishwa na timu mbalimbali, na hasa kinapokaribia kipindi hicho.
Katika hilo, Telegraph imefichua kwamba baadhi ya nyota wa Chelsea hawafurahishwi na mwenendo wa mchezaji mwenzao, Enzo Fernandez, ambaye hivi karibuni alisema hajui nini hatma yake katika viunga vya Stamford Bridge baada ya kuhusishwa na Real Madrid.
Fernandez kwa sasa ndiye nahodha msaidizi wa kikosi hicho cha kocha Liam Rosenior, na amekuwa akikaimu nafasi hiyo kutokana na majeraha ya Reece James. Hata hivyo, hilo halijamzuia kutoa kauli zinazoonyesha kuwa ana uwezekano wa kuondoka mwisho wa msimu huu.
Suala hilo lilianza baada ya kauli zake zisizo na tahadhari kufuatia kipigo cha aibu cha jumla ya mabao 8-2 dhidi ya PSG katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake, alisema: “Sijui, bado kuna mechi nane na FA Cup. Pia Kombe la Dunia, nadhani baada ya hapo tutaona inakuwaje.”
Kauli hiyo iliwatia wasiwasi mashabiki wa Chelsea, hasa baada ya kipigo hicho kikubwa. Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kufanya tena mahojiano, na kusema Jiji la Madrid ni mahali ambapo angependa kuishi siku zijazo.
Zaidi ya hayo, ripoti zinaeleza kuwa Fernandez amekuwa hashirikiani na wenzake katika vyumba vya kubadilishia nguo, wakati huu ambapo kikosi kipo katika kipindi kigumu baada ya kupoteza mechi nne mfululizo katika mashindano yote. Inaelezwa kuwa aliwahi kumkemea na kumrushia mpira kipa Filip Jorgensen kufuatia kosa lake alilofanya katika mechi dhidi ya PSG.
Tabia hiyo imeanza kuwakera wachezaji wenzake, hasa ikichanganyika na dalili za kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake katika kikosi hicho.
Sio wachezaji pekee waliokasirishwa; pia gwiji wa Chelsea, Obi Mikel, alimkosoa mchezaji huyo baada ya mechi dhidi ya PSG.
Akizungumza kupitia podcast yake ya Obi One, alisema: “Kama umechoka, sema wazi uondoke. Hakuna mchezaji aliye mkubwa kuliko klabu, hasa klabu kubwa kama Chelsea.”
Mikel, aliyecheza mechi 372 akiwa na Chelsea aliongeza kuwa kauli na tabia za Fernandez zinaonyesha amekosa heshima kwa klabu na mashabiki.
“Huwezi kusema mambo kama hayo, haijalishi nini kinaendelea. Unalipwa vizuri ili uitumikie klabu; unapaswa kuthamini hilo,” alisema gwiji huyo.
Kwa sasa, hali ndani ya Chelsea inaonekana kuwa tete, huku mustakabali wa Fernandez ukibaki kuwa gumzo kubwa kuelekea dirisha lijalo.