Kocha Chelsea ageuka ‘Mbogo’, akemea mabeki wake
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Stamford Bridge, winga wa Sunderland, Chemsdine Talbi alifunga bao la ushindi dakika ya 93.
LONDON, ENGLAND: WAMEZINGUA. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca amewakemea vikali wachezaji wake wa safu ya beki baada ya kushindwa kucheza vizuri dakika za mwisho na kusababisha kupoteza mechi dhidi ya Sunderland dakika za majeruhi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Stamford Bridge, winga wa Sunderland, Chemsdine Talbi alifunga bao la ushindi dakika ya 93.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco alipokea pasi nzuri kutoka kwa Brian Brobbey, aliyetoa pasi vizuri licha ya kuwa katikati ya mabeki wawili wa Chelsea.
"Ni mpira mrefu tu uliopigwa nyuma ya safu ya beki. Tulikuwa na wachezaji wawili dhidi ya mchezaji mmoja lakini mabeki wetu wa kati hawakucheza inavyotakiwa. Mchezaji aliyepiga pasi alikuwa amegeukia goli lake mwenyewe wakati anapokea mpira, hivyo ilikuwa rahisi kumkaba. Lakini labda tulijaribu kucheza bila ya kuwa makini, pengine ni kwa sababu waliona ni dakika ya 92 au 93 lakini tulipaswa kufanya vizuri zaidi," amesema Maresca.
Kocha huyu ambaye timu yake ilikuwa imeshinda mechi nne mfululizo kabla ya mechi hiyo, amesema hata timu hiyo ilipokuwa inaongoza hakuwa ameridhishwa na namna ilivyokuwa inacheza.
"Hatukucheza vizuri kabisa. Tulikosa ubunifu. Hatukutengeneza nafasi nyingi ukiondoa lile bao tulilofunga. Tuliteseka sana. Tunahitaji wachezaji wetu wote wajitoe kwa asilimia 100. Hata tulipokuwa mbele kwa bao 1-0, tulipoteza mipira mingi."
Maresca pia alifichua Joao Pedro, ambaye amekuwa katika kiwango kibovu katika mechi kadhaa, anasumbuliwa na majeraha ya muda mrefu ya nyonga.
"Joao hajakuwa akifanya mazoezi kila siku kwa sababu ana maumivu ya nyonga na Enzo Fernandez pia ana shida hiyo. Tuna wachezaji wanne hadi watano ambao kwa bahati mbaya kutokana na matatizo fulani, hawawezi kufanya mazoezi kila siku lakini wanajitahidi kucheza mechi.
“Kwa hiyo, Joao katika baadhi ya mechi amekuwa bora, lakini leo aliteseka kidogo ingawa kwangu naona wachezaji wote leo hawakucheza vizuri."
Katika mechi hii ya wikiendi iliyopita, Chelsea ilipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sunderland ambayo imeonekana kuanza ligi vizuri licha ya kupanda daraja msimu huu.