Kiungo ghali kasema... Arsenal ina presha ya ubingwa
Muktasari:
- Arsenal ilijiweka kwenye hatari ya kuanguka pointi nyumbani Jumamosi kabla ya kufunga mara mbili kwenye dakika za majeruhi na kushinda 4-2 dhidi ya Leicester City kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO, Declan Rice amesema mastaa wa Arsenal tayari wameanza kupata presha ya ubingwa ikiwa bado kuna mechi 32 za kucheza.
Arsenal ilijiweka kwenye hatari ya kuanguka pointi nyumbani Jumamosi kabla ya kufunga mara mbili kwenye dakika za majeruhi na kushinda 4-2 dhidi ya Leicester City kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.
Na kiungo huyo ghali kwenye Ligi Kuu England, Rice alisema Arsenal inayopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England imeanza kuwa na presha wakati mechi zikiwa zimebaki 32.
Rice alisema: “Kiakili, ni ngumu sana kuwa na mechi nyingi za kucheza. Kama unataka kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England, unahitaji kushinda, la basi presha utakuwa kubwa. Tunajua tuliingia uwanjani kwenye mechi hii kubwa. Unapoongoza mbili bila, unaona inatosha.
“Unatazama saa na kusema, ‘bado tuna muda’, lakini hapo hapo unakuwa na mawazo mbadala, ‘hatuwezi kuangusha pointi, hatuwezi kupoteza hii mechi, tunaendelea kupambana’. Hupaswi kuangusha pointi kama unataka kushindania taji hadi mwisho wa msimu.”
Baada ya kumalizana na Leicester City, Arsenal ilihamishia nguvu kwenye maandalizi ya mechi yao ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain iliyotarajia kufanyika usiku wa jana Jumanne, huku Jumamosi ijayo wakiwa na kipute cha kukipiga na Southampton.
Gabriel Martinelli na Leandro Trossard waliitanguliza Arsenal kwa mabao kabla ya Leicester City kusawazisha kupitia kwa James Justin, aliyefunga mara mbili, lakini baadaye Wilfred Ndidi alijifunga na Kai Havertz akaihakikishia zaidi The Gunners ushindi baada ya kufunga bao la nne uwanjani Emirates.