Kiungo Chelsea ashambuliwa kwa ubaguzi wa rangi
LONDON, ENGLAND. KIUNGO wa Chelsea, Conor Gallagher ameshambuliwa na kuzomewa kwenye mtandao wa X baada ya kusambaa kwa video yake inayoashiria ubaguzi wa rangi.
Katika video hiyo, Gallagher alionekana kukataa kupeana mkono na mtoto mwenye rangi nyeusi wakati wachezaji wanasalimiana.
Tukio hilo lilitokea kabla ya mchezo dhidi ya Burnley uliomalizika kwa sare ya bao 2-2 kwenye dimba la Stamford Bridge.
Ilikuwa ni wakati wachezaji wa timu zote wanasalimiana kwa kupeana mikono na watoto wanaowasindikiza wachezaji uwanjani kabla ya kuanza mechi.
Hadi sasa Gallagher mwenyewe hajasema chochote kuhusiana na tukio hilo ingawa mashabiki wengi wameonekana kumshambulia.
Staa huyu ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Chelsea na msimu huu amecheza katika mechi 39 za michuano yote.
Tangu dirisha lililopita amekuwa akihusishwa kuondoka kwenye timu hiyo, huku Tottenham ikitajwa kutaka kumsajili.