Kisa waamuzi, Neville amvaa Arteta
Muktasari:
- Kauli ya Neville ni baada ya mwamuzi Michael Oliver kupokea vitisho vya kifo na matusi kutokana na ushindi wa Arsenal wa 1-0 dhidi ya Wolves Jumamosi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United, Gary Neville amemshutumu Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa kuchochea hasira za mashabiki wa Arsenal dhidi ya waamuzi.
Kauli ya Neville ni baada ya mwamuzi Michael Oliver kupokea vitisho vya kifo na matusi kutokana na ushindi wa Arsenal wa 1-0 dhidi ya Wolves Jumamosi iliyopita.
Neville alidai kauli za Arsenal hasa kocha wao huyo, ndizo zilizochochea kuonekana waamuzi wa ligi hiyo wanakula rushwa.
"Wao (mashabiki wa Arsenal) wanatumia maneno kama rushwa, ambayo inamaanisha wanaamini anapewa pesa na kupewa hongo jambo ambalo si kweli."
"Sisi Manchester United tulikuwa na hali ya kuwa na mtazamo wa kushambulia dhidi ya marefa. Arsenal wanafanya kidogo hivyo pia ingawa kwao ni tofauti, hakuna shaka wanachofanya Arsenal kinaongeza mivutano baada ya mechi badala ya kupunguza, wamefanya hivyo kwa miezi 12 sasa."
"Tofauti na sasa ni, mitandao ya kijamii nayo imekuwa kwa kasi sana, wakati sisi tukicheza zamani na kufanyiwa mambo kama haya dhidi ya marefa, hatukuwa tukichochea kile ambacho kingeweza kuwa tuhuma za rushwa kwenye mitandao ya kijamii."
"Sasa Arsenal, kuanzia kwa wachezaji, Mikel Arteta na mashabiki maarufu wamekuwa wakisukuma mambo haya na mbaya zaidi ni hadi kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa tuhuma hizo za rushwa na udanganyifu. Katika nyakati zetu, hatungeweza kuwa na ushawishi mkubwa hivyo, kila mtu alikuwa nyumbani bila simu na hakukuwa na Twitter."
Oliver, ambaye ni mmoja wa marefa wenye uzoefu mkubwa kwenye Ligi Kuu England, alijikuta katikati ya mzozo baada ya kumwonyeshea Myles Lewis-Skelly wa Arsenal kadi nyekundu na uamuzi huo ulizua hasira miongoni mwa mashabiki wa Arsenal, huku tuhuma za upendeleo zikienea haraka mtandaoni.
Hasira hizo zilichukua sura mbaya zaidi, huku Oliver na familia yake, mkewe Laura na binti yao wa miaka miwili wakipokea vitisho vya kifo.