Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa vitisho vya kuuawa agoma kurudi Colombia

COLOMBIA Pict
t

Muktasari:

  • Colombia ilimaliza safari yake ya Kombe la Dunia katika hatua ya 16 Bora baada ya kuchapwa na Uswisi kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.

BOGOTA, COLOMBIA: MSHAMBULIAJI wa Colombia, Jaminton Campaz, anaripotiwa kutorejea nchini kwao baada ya kuondolewa kwenye Kombe la Dunia 2026 kutokana na hofu ya usalama wake kufuatia kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa mashabiki wenye hasira.

Colombia ilimaliza safari yake ya Kombe la Dunia katika hatua ya 16 Bora baada ya kuchapwa na Uswisi kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.

Campaz alikuwa na nafasi ya kuwa shujaa wa taifa lake katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza alipobaki uso kwa uso na kipa, lakini alipiga mpira juu ya lango na kuikosesha Colombia bao la ushindi.

Ingawa baadaye alifanikiwa kufunga penalti yake kwenye mikwaju ya uamuzi, haikutosha kuizuia Colombia kuaga mashindano hayo kwa maumivu.

COLO 05

Vitisho vya kifo vyamwandama

Baada ya kuondolewa, Campaz amekuwa akishambuliwa vikali kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watu wakimtumia ujumbe wa vitisho vya kuuawa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Argentina, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 hakupanda ndege iliyowarejesha nyumbani wachezaji wa Colombia kutokana na hofu ya usalama wake.

Wakati nyota wengine wa Colombia akiwemo James Rodriguez, Davinson Sanchez na Juan Fernando Quintero waliondoka Vancouver kuelekea Bogota Alhamisi asubuhi, Campaz hakuwemo kwenye msafara huo.

Haijafahamika wazi kama alibaki Marekani au alielekea Argentina ambako anakipiga katika klabu ya Rosario Central.

COLO 04

Campaz avunja ukimya

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Campaz aliomba mashabiki watulie na kuheshimu mipaka licha ya maumivu ya kuondolewa.

"Colombia yangu, tafadhali tusipoteze heshima. Tunaweza kuwa na maoni tofauti, kukasirika au kuhuzunika, lakini hakuna mapenzi ya soka yanayopaswa kuhalalisha chuki au watu kuishi kwa hofu," aliandika.

Campaz alisema kuchezea Colombia kwenye Kombe la Dunia ilikuwa ndoto aliyokuwa nayo tangu utotoni.

COLO 01

"Tangu nikiwa mtoto nilitamani kuvaa jezi ya Colombia, kuimba wimbo wa taifa, kuiwakilisha mamilioni ya wananchi na kufunga bao kwenye Kombe la Dunia. Leo namshukuru Mungu kwa kuniruhusu kutimiza ndoto hiyo. Hizi ni kumbukumbu nitakazobeba maisha yangu yote."

Aliwashukuru mashabiki waliowaunga mkono katika safari yao yote ya Kombe la Dunia pamoja na familia yake kwa kuwa nguzo muhimu katika maisha yake.

"Kwa taifa lote la Colombia, naweza kusema ninaumia kama mnavyoumia nyinyi. Sisi pia tulitamani kufika mbali zaidi. Ninasikitika kutowapa furaha ambayo sote tuliitarajia, lakini hakuna wakati ambao nilikosa kujitolea kwa ajili ya taifa langu. Nilitoa kila kitu uwanjani na ningefanya hivyo mara elfu moja zaidi kwa ajili ya nchi yangu."

COLO 03

Kumbukumbu za msiba wa Escobar zafufuka

Sakata hili limeamsha kumbukumbu za tukio la kusikitisha lililoitikisa Colombia katika Kombe la Dunia la mwaka 1994 lililofanyika Marekani.

Beki wa Colombia, Andres Escobar, aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya klabu ya usiku mjini Medellin siku chache baada ya kujifunga katika mechi dhidi ya Marekani, matokeo yaliyoharakisha kuondolewa kwa timu hiyo kwenye mashindano.

Kutokana na vitisho vinavyomkabili Campaz, Shirikisho la Soka la Colombia (FCF) limelaani vikali vitendo hivyo na kuitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzisha uchunguzi wa haraka.

Katika taarifa yake, shirikisho hilo limesisitiza kuwa wahusika wote watambuliwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

COLO 02

"Hakuna mwanamichezo au mtu yeyote anayehusiana naye anayepaswa kutishiwa kwa sababu ya kuiwakilisha nchi yake katika mashindano ya michezo."

FCF iliongeza kuwa soka linapaswa kuwa jukwaa la umoja, heshima na matumaini, si sehemu ya chuki, vitisho au vurugu.

"Soka linapaswa kuunganisha watu. Kushindwa uwanjani hakupaswi kamwe kugeuka kuwa mashambulizi au vitendo vya ukatili katika maisha halisi."