Kisa saa, David Silva kufanyiwa uchunguzi
Muktasari:
- Machi 2022, Silva na kampuni husika walidaiwa kufikia makubaliano na kampuni ilikubali kulipa kodi pamoja na adhabu zote, lakini uchunguzi bado unaendelea ili kubaini kama kulikuwa na mpango wa makusudi wa kukwepa kodi.
CANARIA, HISPANIA: KIUNGO wa zamani wa Manchester City, David Silva anakabiliwa na uchunguzi wa kimahakama unaohusu sakata la saa za kifahari zinazodaiwa kuingizwa bila kulipiwa kodi nchini Andorra.
Silva, ambaye anatokea Gran Canaria, ni miongoni mwa majina mapya ya wanasoka maarufu yaliyotajwa kuhusika katika uchunguzi huo unaohusu ununuzi wa saa za gharama kubwa ambazo huenda ziliingizwa nchini humo kwa njia zisizo rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa, Silva anashukiwa kununua saa nne za chapa ya Patek Philippe kati ya mwaka 2020 na 2021, zenye thamani ya jumla ya takriban Euro 295,000, jambo lililoibua maswali kuhusu uhalali wa miamala hiyo.
Uchunguzi huo unaendelea chini ya jaji nchini Andorra, ukihusisha pia wachezaji wengine waliowahi kucheza katika ligi za Hispania na England, akiwemo Santi Cazorla, Juan Bernat, Cesar Azpilicueta, Giovani Lo Celso na Thomas Partey.
Mamlaka zinachunguza iwapo saa hizo zilinunuliwa na kuhamishwa kati ya Hispania na Andorra bila kutangazwa ipasavyo kwa ajili ya kodi, hali ambayo ingeweza kusababisha ukwepaji wa kodi.
Katika kesi ya Silva, matatizo yake yalidaiwa kuanza Desemba 2020 alipokuwa akiichezea Real Sociedad na alinunua saa yenye thamani ya Euro 120,000. Baadaye aliarifiwa kuhusu deni la VAT la Euro 25,200 pamoja na riba na makubaliano yakafikiwa.
Machi 2022, Silva na kampuni husika walidaiwa kufikia makubaliano na kampuni ilikubali kulipa kodi pamoja na adhabu zote, lakini uchunguzi bado unaendelea ili kubaini kama kulikuwa na mpango wa makusudi wa kukwepa kodi.
Aidha, inachunguzwa iwapo mapato yasiyotangazwa yalitumika kununua mali nyingine kama magari ya kifahari. Hadi sasa, hakuna mashtaka rasmi yaliyothibitishwa dhidi ya Silva au wachezaji wengine.