Kisa Real Madrid, vigogo Bayern wampa muda Davies

VIGOGO wa Bayern Munich wamemwambia beki wa kushoto kutoka Canada, Alphonso Davies hadi wiki ijayo wanataka majibu ikiwa anataka kuwepo kwenye timu hiyo au ataondoka mwisho wa msimu huu.

Kumekuwa na taarifa kwamba Davies anataka kuondoka ili kujiunga na Real Madrid katika dirisha lijalo jambo linalomfanya asisaini mkataba wa kuendelea kusalia.
Bayern inataka kujua staa huyo kama anaondoka ili kuwekeza nguvu zaidi kwenye mchakato wa kumpata mchezaji atakayeziba pengo lake.

Davies amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo kwenye kikosi cha Bayern na mabosi wa timu hiyo wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili asaini mkataba, lakini amekataa.

Mkataba wa sasa wa supastaa huyo mwenye umri wa miaka 23, unamalizika 2025 na katika msimu huu amecheza mechi 31 za michuano yote na kutoa asisti tatu.