Kisa McTominay... Scotland yamshukuru Jose Mourinho
Muktasari:
- Na alikuwa Mourinho aka ‘The Special One’ ndiye aliyemsaidia McTominay kupita kwenye njia sahihi hadi sasa kuwa shujaa wa Scotland baada ya kumpika vyema walipokuwa wote Old Trafford.
EDINBURGH, SCOTLAND: SCOTT McTominay amesubiri muda mrefu kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza Manchester United chini ya kocha Jose Mourinho.
Na alikuwa Mourinho aka ‘The Special One’ ndiye aliyemsaidia McTominay kupita kwenye njia sahihi hadi sasa kuwa shujaa wa Scotland baada ya kumpika vyema walipokuwa wote Old Trafford.
Kiungo huyo anayekipiga Napoli kwa sasa amekuwa gumzo siku za hivi karibuni baada ya kuiwezesha Scotland kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa mara ya kwanza tangu 1998 baada ya kufunga bao la kwanza kwa staili maridadi sana katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Denmark.
Baada ya kuondoka Manchester United na kwenda Napoli, ambako alionyesha kiwango bora sana, akiisaidia timu hiyo kushinda taji la Serie A msimu uliopita, huku akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka huko Italia.
Kwa nyakati zake alizokuwa kwenye Ligi Kuu England, hakuwa na maajabu sana, lakini McTominay alionyesha kuwa kwenye beji lake kumejaa kipaji kikubwa.
Mourinho aliliona hilo na alishangaa kuona England inachukua muda mrefu haimjumuishi kwenye kikosi chao cha timu ya taifa, Three Lions.
Na England kwa wakati huo iliyokuwa chini ya kocha Gareth Southgate iliposhindwa kufanya haraka kumchukua kiungo huyo akachezee Three Lions, Mourinho badala yake aliwashtua Scotland kwa kuwafanya wafahamu kwamba mlango upo wazi kwao kwenda kumchukua staa huyo.
McTominay alikuwa anafuzu kuichezea Scotland kimataifa kupitia baba yake mzaliwa wa Helensburgh na kwa kipindi hicho, Alex McLeish, ndiye aliyekuwa kocha wa Scotland.
Wakati McLeish alipopata taarifa hiyo kwamba anaweza kumvuta McTominay kwenda kuichezea timu ya taifa ya Scotland, hakujichelewesha kumfuata, licha ya safari yake ya kumfikia staa huyo mazoezini Carrington, ilikumbana na vikwazo vingi vya hali ya hewa.
McLeish alisema: “Nikitazama huko tulikotoka, sisi Waskochi tunapaswa kumshukuru sana Jose Mourinho. Jose alifanya mahojiano wakati alipowaambia England wanajiweka kwenye hatari ya kumkosa Scott na hapo ndipo nilipopata nafasi ya kwenda kukutana naye kwa mara ya kwanza!
“Hivyo nilijiandaa kwenda kwenye uwanja wa mazoezi wa Man United kwenda kuonana na Scott. Kulikuwa na tatizo moja, hali ya hewa haikuwa nzuri, ilikaribia kabisa nisifanikiwe kumfikia!
“Nilichelewa kufika na nilifikiria hata kuahirisha na kurudi, hali ya hewa ilikuwa mbaya. Niliamua hadi kurudi hotelini kwangu Manchester Piccadilly, nilikuwa na wasiwasi hata wa kukosa chumba. Bahati nzuri nilipata chumba!”
Mourinho alikuwa tayari kuwapa Scotland kila nafasi ya kumfikia McTominay ili kupata nafasi ya kwenda kuitumikia timu ya taifa. Na hakika, staa huyo amelipa fadhila hiyo, kwa kufunga bao maridadi kabisa katika kuifanikisha Scotland katika fainali za Kombe la Dunia 2026, ambazo zitafanyika huko Marekani, Canada na Mexico.
McLeish aliongeza: “Nilimpigia Jose kesho yake asubuhi. ‘Njoo hapa saa 6, tutapata mlo wa mchana pamoja na nitazungumza na Scott hivyo atakuwepo’. Haikuwa shida. Niliona Scott yupo tayari, lakini bado nilikuwa naona kuna kazi kubwa ya kumshawishi. Alikuja na tayari akili yake ilikuwa wazi kabisa kwamba alitaka kuichezea timu ya taifa ya Scotland.”