Barnes, Gordon waiongoza Newcastle kuichapa Benfica ya Mourinho
Muktasari:
- Gordon, ambaye hakuwa akilindwa, alifungua ukurasa wa mabao kipindi cha kwanza kwa kutuliza mpira na kuumimina wavuni akimshinda kipa wa Benfica, Anatoliy Trubin, baada ya kupokea pasi ya Jacob Murphy iliyopita mbele ya lango.
NEWCASTLE, ENGLAND: Harvey Barnes na Anthony Gordon wameipa Newcastle United ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Benfica inayoongozwa na Jose Mourinho katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ikichezwa St James' Park, usiku wa Oktoba 21, 2025.
Gordon, ambaye hakuwa akilindwa, alifungua ukurasa wa mabao kipindi cha kwanza kwa kutuliza mpira na kuumimina wavuni akimshinda kipa wa Benfica, Anatoliy Trubin, baada ya kupokea pasi ya Jacob Murphy iliyopita mbele ya lango.
Hilo lilikuwa bao la nne kwa Gordon katika mechi tatu za mashindano hayo na likawapa Newcastle motisha ya kusaka mengine zaidi kipindi cha pili.
Barnes aliongeza bao la pili baada ya kipa Nick Pope kutupa mpira mrefu kuelekea upande wa kulia.
Beki wa Benfica, Antonio Silva, alikosea kuumudu mpira huo na Barnes akauwahi, kisha akafunga kwa mpira uliogonga mwamba kabla ya kuingia wavuni.
Kabla ya filimbi ya mwisho, Barnes alipachika bao la tatu na kukamilisha ushindi baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Gordon, kisha akampiga chenga kipa Trubin na kupenyeza mpira kupitia miguu yake.
Benfica itasikitika kwa nafasi ilizopoteza, kwani ilikaribia kufunga mara mbili kipindi cha kwanza, Pope akiuokoa mkwaju wa Dodi Lukebakio kwa mkono, kisha Lukebakio huyo huyo akagonga mwamba dakika chache baadaye kwa shuti kali kutoka nje ya boksi.
Hata hivyo, Gordon na Barnes waliitumia vyema kila nafasi waliyopata, na Newcastle ikaandika historia ya kupata ushindi wa pili mfululizo katika Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2003 na kufikisha pointi sita ikikamata nafasi ya saba kwenye msimamo.