Kinda Real Madrid amtaja Messi mchezaji wake bora namba moja
Muktasari:
- Mastantuono, mwenye umri wa miaka 18, amekuwa sehemu ya kikosi cha Real Madrid alichojiunga nacho msimu huu akitokea River Plate ya kwao Argentina.
Nyota chipukizi wa Real Madrid, Franco Mastantuono, amemtaja Lionel Messi kama mchezaji wake bora namba moja anayemvutia.
Katika orodha yake hiyo ya wachezaji watatu wanaomvutia, Mbali na Messi, kuna Jude Bellingham na Julián Álvarez.
Mastantuono, mwenye umri wa miaka 18, amekuwa sehemu ya kikosi cha Real Madrid alichojiunga nacho msimu huu akitokea River Plate ya kwao Argentina.
Ndani ya Real Madrid, amecheza mechi saba za La Liga akifunga bao moja. Pia amecheza mechi mbili za UEFA na kutoa asisti moja. Kwa sasa yupo kambini na timu ya taifa ya Argentina kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Venezuela na Puerto Rico.
Akizungumza na ESPN, winga huyo ameeleza uzoefu wake na kuwataja wachezaji watatu waliomvutia zaidi tangu aingie katika soka la ushindani.
“Wachezaji watatu wananiovutia zaidi. Kwanza, Leo [Messi]. Halafu Bellingham amenivutia sana. Ni mchezaji mkubwa, hasa mazoezini, niliona kuwa ana utofauti na wachezaji wengine.
"Mwisho, Julián [Álvarez]. Nililazimika kuteseka naye kwenye mechi iliyopita,” amesema
Winga huyo ameeleza jinsi alivyoathiriwa na kiwango cha Bellingham mazoezini ndani ya kikosi cha Real Madrid, akithibitisha kuwa ameshuhudia uwezo mkubwa wa Mwingereza huyo.
Kwa Mastantuono, Lionel Messi ndiye chaguo la kwanza anayemvutia zaidi. Kwa sasa, watu wengi wamekuwa wakimlinganisha Mastantuono na Messi, hasa baada ya kuvaa jezi namba 10 ya Messi wakati wa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Ecuador mwezi uliopita, ambapo staa huyo hakuwepo.
Kama ilivyo kwa Messi, Julián Álvarez pia amemvutia Mastantuono kwa kiwango chake bora. Álvarez, ambaye aliwahi kuchezea River Plate kabla ya kuhamia Ulaya, yupo katika kiwango cha juu msimu huu akiitumikia Atletico Madrid.
Mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili dhidi ya Real Madrid katika ushindi wa 5-2 ilioupata Atlético Madrid, Septemba 2025, mechi ambayo Mastantuono alikuwa mpinzani wake.