Kimmich afichua siri kubaki Bayern

Muktasari:
- Mkali huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi ndani ya uwanja tayari ameshatumika mara 39 msimu huu na amekuwa hakosi namba kwenye kikosi kinachoanza cha kocha huyo Mbelgiji.
MUNICH, UJERUMANI: KIUNGO fundi wa mpira, Joshua Kimmich amefichua kwamba sababu ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Bayern Munich kwa vile ni mahali anapoamini atafanikiwa kuliko kwenda kwingineko.
Staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani mkataba wake ulikuwa unafika ukomo mwisho wa msimu huu na kulikuwa na klabu kibao zinamtaka, ikiwamo za Ligi Kuu England ambazo ni Arsenal na Newcastle United. Lakini, sasa Kimmich amekubali kusaini mkataba mpya wa kubaki Bayern hadi 2029 akiendelea kutamba Allianz Stadium na kuzima kabisa uvumi wa kuachana na timu hiyo.
Kimmich, 30, ameendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha kocha Vincent Kompany, ambacho kimetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, huku kikiongoza pia kwa tofauti ya pointi nane kwenye msimamo wa Bundesliga.
Mkali huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi ndani ya uwanja tayari ameshatumika mara 39 msimu huu na amekuwa hakosi namba kwenye kikosi kinachoanza cha kocha huyo Mbelgiji.
Kimmich alijiunga na Bayern akitokea RB Leipzig mwaka 2015 na kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho ina maana anataka kuendelea kuvuna kile ambacho amekuwa akivuna na miamba hiyo. Kimmich alisema wachezaji wenzake na mazingira mazuri kwenye timu hiyo ndicho kilichomshawishi kubaki.
"Hapa FC Bayern, kuna mazingira bora kabisa ya kufikia malengo yangu kwenye michezo," alisema.
"Nilifanya uamuzi wangu kwa kuzingatia hilo. Kwa sasa kuna wachezaji wazuri, makocha wazuri na mazingira mazuri ya klabu yanayokupa uhakika wa kufanikiwa. Nadhani najisikia vizuri kuwa hapa, kuna vitu bado sijavimaliza."
Klabu imefurahia kukamatia saini ya Kimmich baada ya mkurugenzi mtendaji mkuu, Jan-Christian Dreesen kusema: "Tumefurahi Joshua Kimmich anaendelea kubaki FC Bayern. Ni mtu ambaye siku zote amekuwa akituongoza, iwe kwenye klabu au timu ya taifa."
Kimmich amefuata nyayo za mastaa wenzake Manuel Neuer, Jamal Musiala na Alphonso Davies ambao wamesaini mikataba mpya ya kuendelea kukipiga Bayern.