Kimbunga chaitingisha England Kombe la Dunia
Muktasari:
- Nyota wa England walikuwa wamewasili Kansas City asubuhi ya Jumamosi na kufanya mazoezi yao ya kwanza katika uwanja wa Swope Soccer Village huku wakionekana kufurahia hali nzuri ya hewa iliyokuwa na jua.
KANSAS CITY, MAREKANI: WACHEZAJI wa timu ya taifa ya England wamejikuta wakilazimika kujifungia ndani baada ya mamlaka za hali ya hewa nchini Marekani kutoa tahadhari ya dharura kuhusu uwezekano wa kutokea kwa kimbunga hatari aina ya tornado karibu na kambi yao ya Kombe la Dunia 2026.
Nyota wa England walikuwa wamewasili Kansas City asubuhi ya Jumamosi na kufanya mazoezi yao ya kwanza katika uwanja wa Swope Soccer Village huku wakionekana kufurahia hali nzuri ya hewa iliyokuwa na jua.
Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla jioni ya siku hiyo baada ya mawingu mazito kutanda, yakifuatana na radi kali, ngurumo za kutisha, mvua kubwa pamoja na upepo mkali uliokuwa ukivuma kwa kasi ya hadi maili 80 kwa saa.
Tahadhari maalumu ilitolewa kupitia simu kwa wakazi wote wa eneo hilo, wakiwemo wachezaji wa England, ikiwataka kutafuta hifadhi ya haraka ndani ya majengo imara na kujiepusha na madirisha kutokana na hatari ya mabaki yanayoweza kurushwa na upepo mkali.
Ujumbe huo wa dharura ulionya kuwa mabaki yanayobebwa na upepo yanaweza kuwa hatari kwa maisha ya watu walioko nje bila kinga huku pia ukiwataka wananchi kuelekea katika vyumba vya ndani vilivyopo ghorofa za chini za majengo.
Mamlaka ya Kitaifa ya Hali ya Hewa ya Marekani ilitangaza kuwa tahadhari ya uwezekano wa tornado ingeendelea kutumika hadi usiku katika maeneo ya Kansas na Missouri ambako England imeweka kambi yake.
Kutokana na hali hiyo, kikosi kizima cha England kilifuata maelekezo ya usalama na kubaki ndani ya majengo huku kikisubiri hali ya hewa kutengamaa.
England inatumia makao ya klabu ya Sporting Kansas City kama kituo chake cha mazoezi wakati wa mashindano haya, huku wachezaji wakifikia katika hoteli ya The Inn at Meadowbrook iliyoko kusini mwa jiji hilo.
Cha kushangaza ni kwamba saa chache kabla ya tahadhari hiyo, mazingira yalikuwa tofauti kabisa. Wachezaji walifanya mazoezi mbele ya mashabiki wapatao 300 waliokuwa wamejitokeza kushuhudia maandalizi ya kikosi hicho.