Neymar afanya kufuru Florida
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, watu wa karibu wa Neymar wanaishi katika jumba la kifahari la vyumba 14 linalokadiriwa kuwa na thamani ya pauni 10.8milioni (zaidi ya sh 35 bilioni).
FLORIDA, MAREKANI: TUMIA hela ikuzoee. Nyota wa Brazil, Neymar amefanya kufuru baada ya taarifa kuibuka kuhusu maisha ya anasa anayoyaishi na msafara wake wakati wa michuano ya Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, watu wa karibu wa Neymar wanaishi katika jumba la kifahari la vyumba 14 linalokadiriwa kuwa na thamani ya pauni 10.8milioni (zaidi ya sh 35 bilioni).
Jumba hilo, lililopo eneo la Eagle Cove ndani ya Reunion Resort, Florida, Marekani, linatajwa kupangishwa kwa pauni 2,900 kwa siku (zaidi ya sh 9.5milioni).
Eneo hilo la kifahari liko umbali wa dakika 20 kwa gari kutoka Disney World, likiwa sehemu maarufu kwa makazi ya matajiri na wageni wenye mkwanja mrefu wanaotembelea Florida.
Inasemekana kuwa nyumba hiyo imekodishwa na baba yake Neymar, Neymar Santos Sr. ambaye mara nyingi huambatana na mwanawe.
Jumba hilo la kifahari lina huduma nyingi za kisasa zinazolifanya kuwa zaidi ya makazi ya kawaida ya muda mfupi. Ndani yake kuna chumba cha michezo mbalimbali chenye televisheni kubwa.
Kwa upande wa michezo na mazoezi, mjengo huo una gym ya kisasa, bwawa kubwa la kuogelea, uwanja wa mpira wa kikapu, pamoja na sehemu ya mazoezi ya gofu na hata uwanja mdogo (bowling).