Refa Msomali kulipwa mamilioni na FIFA
Muktasari:
- Artan ambaye alikuwa ameandika historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuchaguliwa kuchezesha Kombe la Dunia, alizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami alipowasili kutoka Istanbul, Uturuki.
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limeamua kumlipa mwamuzi wa Somalia, Omar Artan, fedha zote alizostahili kupata katika Kombe la Dunia 2026 licha ya kushindwa kushiriki mashindano hayo baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani.
Artan ambaye alikuwa ameandika historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuchaguliwa kuchezesha Kombe la Dunia, alizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami alipowasili kutoka Istanbul, Uturuki.
Baada ya mahojiano ya muda mrefu yaliyodumu saa 11, alinyimwa kuingia nchini humo na kurejeshwa Uturuki.
Licha ya tukio hilo, FIFA imeonyesha kumuunga mkono kwa kuthibitisha kuwa atapokea malipo yote ya mashindano pamoja na bonasi ambazo waamuzi wengine wanaoshiriki Kombe la Dunia wanapokea.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za awali kuhusu mfumo wa malipo ya waamuzi wa Kombe la Dunia, waamuzi wa kati hulipwa mkwanja unaokadiriwa kufikia dola 70,000 hadi 100,000 (zaidi ya Sh 180 hadi 260 milioni) huku wakipata bonasi za ziada kwa kila mechi wanayochezesha ambazo zinaweza kufikia kati ya dola 3,000 na 10,000 kulingana na hatua ya mashindano.
Artan mwenye umri wa miaka 34 ni mmoja wa waamuzi bora zaidi barani Afrika na mwaka 2025 alitwaa tuzo ya Mwamuzi Bora wa Afrika kutoka CAF.
Kabla ya kuzuiwa kuingia Marekani, alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 walioteuliwa na FIFA kusimamia mechi za Kombe la Dunia 2026.
Mamlaka za Marekani zilisema mwamuzi huyo alikataliwa kuingia nchini kutokana na kile walichokiita 'masuala ya uhakiki wa kiusalama' (vetting concerns) huku maofisa wengine wakidai kulikuwa na taarifa zinazomhusisha na watu wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na makundi ya kigaidi.
Artan amekanusha madai hayo na kusisitiza hana uhusiano wowote na makundi hayo. Wakati ndoto yake ya kuchezesha Kombe la Dunia ikivunjika ghafla, mwamuzi huyo amepata faraja baada ya UEFA na CAF kumteua kuchezesha mechi ya UEFA Super Cup itakayopigwa Agosti mwaka huu kati ya PSG dhidi ya Aston Villa.