Kila mtu na lake pale La Liga

MADRID, HISPANIA. LIGI Kuu Hispania (LaLiga) inarejea tena wikiendi hii baada ya kusimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), huku kila timu ikiwa na lake kutokana na msimamo wa ligi ulivyo.

Ukianzia kwa Atletico Madrid inayoshika nafasi ya tano kwa pointi zao 55, itakuwa inahitaji kushinda mechi ijao ili kuingia kwenye nafasi nne za juu zitakazoiwezesha kufuzu Ligi ya Mabigwa Ulaya msimu ujao.

Mbali ya kuhitaji kushinda, pia itakuwa inaiombea matokeo mabaya Athletic Club inayoshika nafasi hiyo kwa pointi 56, ipoteze mechi dhidi ya vinara wa ligi, Real Madrid.

Nafasi ambayo Atletico inaishika ikiwa itamaliza hapo itawawezesha kufuzu michuano ya Europa League mwakani.

Wakati Atletico ina hilo, Real Betis ambayo inashikilia nafasi ya saba ina lake.

Timu hii ina pointi 42, mechi ijayo itakuwa ugenini kucheza na Girona. Nafasi waliyopo haiwawezeshi kufuzu michuano yoyote ya Ulaya, hivyo wanahitaji kushinda kwa namna yoyote ili kufikisha pointi 45 ambazo zitawawezesha kupunguza pengo la alama kati yao na  Real Sociedad yenye pointi 46.

Kushinda kwenye mechi hiyo hakutotosha bali watatakiwa waiombee mabaya Socided kwenye mechi yao dhidi ya Alves watoe sare ama wapoteze ambapo lile pengo la alama litapungua hadi moja kama ikifungwa ama mbili kama ikitoa sare.

Timu zinazoshika nafasi za chini kila mtu pia ana lake. Cadiz inayoshikilia nafasi ya 18 katika mstari mwekundu wa kushuka daraja kwa pointi zao 22, itatakiwa kushinda mechi mbili zijazo na kuiombea Celta Vigo ifanye vibaya pia kwenye mechi mbili zijazo ili kuishusha na wao kupanda hadi nafasi ya 17.

Mbali ya kuiombe mabaya Celta Vigo, pia itatakiwa kufanya  hivyo kwa Sevilla ambayo ina pointi 28, ikishinda mechi mbili hizo itakuwa na idadi ya pointi sawa nao kama hawatofanya vizuri kwenye mechi mbili na Cadiz inaweza kupaa hadi nafasi ya 16 kwa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kupoteza mechi mbili kwa Celta Vigo na Sevilla inawezekana kwa sababu zote zitakutana na timu ambazo zipo juu yao kwenye mechi hizo mbili zijazo.

Vilevile kwa upande wa vinara Real Madrid ambao tofauti ya alama kati yao na Barcelona  ni nane tu, presha kubwa waliyonayo kwa sasa ni kutoangusha pointi kwenye mechi tisa zilizosalia kwani ikicheza vibaya karata zao kuna uwezekano ikajikuta ikiondolewa kileleni kwenye dakika za mwisho za ligi hiyo.

Vilevile Girona inayoonekana kuwa na asilimia nyingi za kumaliza kwenye nafasi nne za juu, nayo kwa sasa ina presha ya kuhitaji isiangushe pointi kwani utofauti wa alama kati yake na Atletico iliyopi nafasi ya tano ni pointi saba tu, jambo ambalo linaweza kusababisha watolewe kwenye nafasi yao ikiwa itafanya vibaya kwenye mechi tatu kati ya tisa zilizobaki.