Kigogo Dortmund athibitisha ishu ya Sancho
Muktasari:
- Baada ya hapo, Sancho alijiunga na Aston Villa kwa mkopo, lakini bado hajarejea katika kiwango chake bora, akiwa amefunga bao moja tu.
DORTMUND, UJERUMANI: BOSI wa Borussia Dortmund, Lars Ricken ameweka wazi klabu hiyo bado ina nia ya kumsajili tena kwa mara ya tatu winga wa Manchester United, Jadon Sancho.
Sancho, ambaye alinunuliwa na Man United kwa Pauni 73 milioni mwaka 2021, amekuwa na kipindi kigumu Old Trafford na katika mechi 83 alizoichezea akiwa na mashetani hao wekundu, amefunga mabao 12 pekee, huku akitumia misimu miwili na nusu iliyopita akiwa kwa mkopo.
Alirejea Dortmund kwa nusu ya pili ya msimu wa 2023/24, kabla ya kwenda Chelsea msimu uliopita. Chelsea ilikuwa na kipengele cha kumsajili mazima ikiwa ingehitaji lakini ilisita kufanya hivyo na badala yake ililipa faini ya Pauni 5 milioni.
Baada ya hapo, Sancho alijiunga na Aston Villa kwa mkopo, lakini bado hajarejea katika kiwango chake bora, akiwa amefunga bao moja tu.
Mkataba wake na Man United unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na Man United imeamua kutotumia kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi, hivyo ataondoka akiwa huru.
Ricken amesema Sancho bado ni miongoni mwa wachezaji wanaowatazama kwa sasa na ikiwezekana watamsajili mwisho wa msimu.
Akizungumza na Sport Bild amesema: "Kwa sasa tunaangalia wachezaji wengi na kuwachambua. Tunaangalia kama wanaweza kutufanya kuwa bora zaidi. Tunafanya hivyo pia kwa Jadon.”
Aliongeza; wanatafuta mchezaji wa kushambulia mwenye ubora, anayeweza kusaidia timu haraka bila gharama kubwa ya uhamisho.
Sancho amekuwa na msimu mgumu akiwa Villa, akianza mechi 17 tu katika mashindano yote. Bao lake pekee alifunga katika Europa League dhidi ya Fenerbahce kwenye ushindi wa bao 1-0.