Man United ni Baleba, Wharton, Anderson tu
Muktasari:
- Kocha Ruben Amorim anataka kuendeleza harakati zake za kunyakua wachezaji ambao tayari wameshaonyesha kitu kwenye Ligi Kuu England, huku kipaumbele chake kikubwa dirisha lijalo la usajili ni kunyakua viungo wa kati.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeweka ubaoni orodha ya viungo watatu, Adam Wharton, Elliot Anderson na Carlos Baleba ikiwa ni mpango wa kuboresha eneo hilo la kati ya uwanja.
Kocha Ruben Amorim anataka kuendeleza harakati zake za kunyakua wachezaji ambao tayari wameshaonyesha kitu kwenye Ligi Kuu England, huku kipaumbele chake kikubwa dirisha lijalo la usajili ni kunyakua viungo wa kati.
Mabosi wa klabu hiyo kwa sasa wanatazama ni kiungo gani atakwenda kufiti kwenye mfumo wa kocha Amorim na ndiyo maana imeweka ubaoni majina matatu. Kiungo wa Nottingham Forest, Anderson ameonyesha kiwango bora sana hata kwenye timu ya taifa ya England wakati wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 chini ya Kocha Thomas Tuchel.
Man United inamfukuzia pia Wharton wa Crystal Palace na ilikaribia kumsajili staa wa Brighton, Baleba dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Kama klabu hizo tatu zitahitaji pesa nyingi dirisha la Januari, basi Man United itakuwa tayari kusubiri hadi wakati wa dirisha la majira ya kiangazi kuliko kwenda kusajili mchezaji wa nje ya Ligi Kuu England.
Man United inaona umuhimu wa kusajili wachezaji walionyesha kitu kwenye Ligi Kuu England baada ya kupata huduma nzuri kutoka kwa Matheus Cunha na Bryan Mbeumo waliosajiliwa kutoka Wolves na Brentford mtawalia dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Mbeumo, aliyenaswa kwa Pauni 71 milioni ndiye kinara wa mabao wa Man United hadi sasa msimu huu, akifunga mara sita, wakati Cunha, aliyesajiliwa kwa Pauni 62.5 milioni, amekuwa muhimu katika safu mpya ya ushambuliaji ya kocha Ruben Amorim.
Baada ya usajili wa Pauni 80 milioni ya beki wa kati Harry Maguire kutoka Leicester City mwaka 2019, mchezaji mwingine pekee aliyesajiliwa na Man United kutoka kwenye Ligi Kuu England kabla ya Cunha aliyetua Juni mwaka huu, alikuwa Mason Mount kutoka Chelsea mwaka 2023. Sasa mpango wa Man United ni kusajili viungo.
Dirisha lililopita, Man United ilitumia zaidi ya Pauni 200 milioni kuwasajili Mbeumo, Cunha, straika Benjamin Sesko, kipa Senne Lammens aliyesajiliwa kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi wakati Patrick Dorgu alinaswa Januari.
Man United itakuwa na pesa ya kutosha kuwekeza kwenye sehemu ya kiungo mwishoni mwa msimu huu kutokana na kuwapo na uwezekano wa Casemiro kuondoka la kama atapunguza mhshahara wake ili asainishwe dili jipya. Casemiro, ambaye atafikisha umri wa miaka 34, Februari mwakani, mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu.
Man United haionekani kuwa na mpango wa kumwongezea mwaka mwingine Casemiro endapo kama hatashusha mshahara, wakati sasa akiwa miongoni mwa mastaa watatu wanaolipwa zaidi ya Pauni 300,000 kwa wiki. Jadon Sancho, ambaye ni mmoja wa wanaolipwa pesa nyingi, Pauni 250,000 kwa wiki, atatemwa Juni mwakani. Kuwaondoa Sancho na Casemiro, Man United itakuwa imeokoa zaidi ya Pauni 31 milioni kwa mwaka kwenye mishahara.
Pesa nyingine zitapatikana kwa kuwaondoa Tyrell Malacia, huku Man United ikilenga kupokea Pauni 38 milioni kutoka Napoli, ambao watamchukua Rasmus Hojlund jumla, huku Barcelona nayo itajiandaa kulipa Pauni 30 milioni kumsajili Marcus Rashford, ambaye mshahara wake Pauni 325,000 kwa wiki, kutokana na mkopo wake kuwa muhimu huko Nou Camp na amefunga mabao sita na asisti tisa katika mechi 16.