Sancho anavyopuna pesa Man United
Muktasari:
- Mwisho wa msimu winga huyo atakuwa ametumia muda sawa akiwa kwa mkopo katika klabu nyingine kama alivyotumia ndani ya Man United.
MANCHESTER, ENGLAND: JADON Sancho ameonekana kuwa kosa la gharama kubwa sana tangu aliposajiliwa na Manchester United.
Mwisho wa msimu winga huyo atakuwa ametumia muda sawa akiwa kwa mkopo katika klabu nyingine kama alivyotumia ndani ya Man United.
Sancho mwenye umri wa miaka 25 yuko kwenye mkopo wake wa tatu nje ya Man United baada ya kujiunga na Aston Villa wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo Chelsea na kuisaidia timu hiyo kushinda taji la UEFA Europa Conference League, lakini Chelsea hawakushawishika kufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu. Mkopo wake wa kwanza ulikuwa mwaka 2024 aliporudi Borussia Dortmund.
Sancho alinunuliwa na Man United kwa ada kubwa ya Pauni 73 milioni akitokea Dortmund mwaka 2021.
Lakini hiyo ni sehemu tu ya fedha ambazo mchezaji huyo wa zamani wa akademi ya Manchester City ameigharimu Man United. Aliichezea klabu hiyo mara 83, akifunga mabao 12 na kutoa asisti sita tu. Wakati huo huo alikuwa akipokea mshahara wa takribani Pauni 250,000 kwa wiki, ingawa kiasi hicho kilipungua baada ya Man United kushindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man United pia ililazimika kulipa malipo ya Pauni 17 milioni huko Dortmund majira ya joto yaliyopita, jambo lililothibitishwa na Jim Ratcliffe.
Hii imefanya matumizi yote ya Man United kwa Sancho kufikia karibu Pauni 100 milioni, hata baada ya sehemu ya mshahara wake kulipwa na klabu alizokuwa kwa mkopo. Man United iliweza kurejesha karibu Pauni 5 milioni kupitia ada ya mkopo kutoka Chelsea.
Mkataba wa Sancho katika kikosi cha Old Trafford unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na na inaaminika hatapewa mkataba mpya.
Winga huyo aliwahi kuhusishwa na uhamisho kwenda Italia katika klabu ya AS Roma majira ya joto yaliyopita, lakini dili hilo halikukamilika na badala yake akaenda kwa mkopo Aston Villa. Tangu ajiunge na klabu hiyo ya Villa Park, Sancho amecheza mechi 28 na kufunga bao moja.
Sancho alifika Man United baada ya kung’ara sana akiwa Borussia Dortmund, ambapo alikuwa na rekodi bora ya mabao na pasi za mabao licha ya kuwa na umri mdogo. Katika miaka yake minne ya kwanza, alifunga zaidi ya mabao 50 na kutoa asisti zaidi ya 50.