Keane amwambia Mainoo: Kaza!
Muktasari:
- Mainoo bado anasubiri nafasi ya kuanzishwa kwenye mechi ya Ligi Kuu England msimu huu, huku kitendo chake cha kuwekwa benchi na kocha Amorim kikizua mjadala mzito kwa miezi ya karibuni.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO gwiji wa Manchester United, Roy Keane amemtaka Kobbie Mainoo kumthibitishia Kocha Ruben Amorim anafanya makosa kumweka benchi kwa kuhakikisha anapambana kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo.
Mainoo bado anasubiri nafasi ya kuanzishwa kwenye mechi ya Ligi Kuu England msimu huu, huku kitendo chake cha kuwekwa benchi na kocha Amorim kikizua mjadala mzito kwa miezi ya karibuni.
Kaka wa kiungo Mainoo, 20, Jordan Mainoo-Hames alikuwa gumzo Jumatatu iliyopita wakati alipovaa fulana iliyoandikwa “Free Kobbie Mainoo” kifuani wakati Man United ilipotoka sare ya mabao 4-4 dhidi ya Bournemouth.
Mainoo, ambaye alishangiliwa sana na mashabiki wa Man United wakati alipoingia katika mechi hiyo akitokea benchini, alishuhudia maombi yake ya kutaka kuondoka Old Trafford kwa mkopo dirisha lililopita la majira ya kiangazi yakigonga mwamba kabla ya sasa kuhusishwa pia na mpango wa kutaka kuondoka wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa.
Nahodha wa zamani wa Man United, Keane amesema: “Mnaniambia hawezi kuwapo hapo kwa miezi mingine sita? Kwamba asifikirie kocha anaweza kuondoka mwisho wa msimu au mchezaji mmoja au wachezaji wawili wa kikosi cha kwanza wataondoka. Umri wake ni miaka 20 kuna ubaya gani wa kukaa na kujifunza? Na hata kama hupati nafasi, kuna namna tofauti ya kukufanya ufikie viwango. Wakati mwingine kocha anaweza kuwa tatizo, hivyo unachopaswa kufanya ni kumfanya kocha aone anakosea kukuweka benchini.”
Keane aliongeza: “Kila siku ni mtihani kwako kumthibitishia kocha wakati anapofanya uteuzi wa kikosi chake, unapaswa ufanye mazoezi kwa nguvu zote kuhakikisha jina lako linakuwapo kwenye orodha ya wanaoanza. Hilo linapaswa kuwa akilini. Kuwa na kaka anayefanya vitu vya kijinga kama vile, hakupaswa kupewa nafasi. Wakati mwingine tunazungukwa na wajinga, hasa hizi familia zetu.”
Hivi karibuni, kocha wa Man United, Amorim amesema Mainoo anagombea namba na Bruno Fernandes. Mainoo anaweza kupata nafasi ya kucheza Jumapili dhidi ya Aston Villa kutokana na Casemiro kutumikia adhabu alipoonyeshwa kadi ya tano kwenye mechi dhidi ya Bournemouth, Jumatatu iliyopita.