Mbio za ubingwa EPL zashika kasi baada ya vipigo Ulaya
Muktasari:
- Sifa ya Premier League kuwa ligi bora zaidi barani Ulaya ilipata pigo kubwa ndani ya saa 48 wiki hii, baada ya timu sita hakuna hata moja iliyocheza hatua ya 16 bora ilishinda mchezo wake.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya wiki ngumu barani Ulaya kwa klabu za England, timu hizo zinarejea katika majukumu ya Ligi Kuu England leo huku mbio za ubingwa na kuepuka kushuka daraja zikifikia hatua muhimu.
Sifa ya Premier League kuwa ligi bora zaidi barani Ulaya ilipata pigo kubwa ndani ya saa 48 wiki hii, baada ya timu sita hakuna hata moja iliyocheza hatua ya 16 bora ilishinda mchezo wake.
Manchester City ilikuwa moja ya timu nne zilizopata kipigo, na italazimika kujipanga haraka baada ya kufungwa mabao 3-0 na Real Madrid. Sasa itakutana na West Ham United ugenini leo Jumamosi, wakati ambapo inaweza kujikuta ikiendelea kuwa nyuma ya kinara Arsenal kwa zaidi ya pointi saba zilizopo sasa endapo itafanya tena vibaya kwenye mchezo huo.
City ilizidiwa kwa sehemu kubwa katika dimba la Santiago Bernabéu na itahitaji kurejea kwa kiwango cha ajabu katika mchezo wa marudiano ili kuokoa matumaini yake ya Ulaya. Hata hivyo, kwanza lazima ihakikishe haipati pigo lingine litakalohatarisha ndoto zake za ubingwa wa Premier msimu huu.
Tayari kocha wa City Pep Guardiola ameshasema kuwa anaona hatari mbele yake kutokana na ratiba kuwa ngumu kwao, lakini ni wakati sasa wa wachezaji wake kuonyesha ukubwa uwanjani.
Timu hiyo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 60 baada ya kucheza michezo 29, zikiwa ni saba nyuma ya Arsenal iliyocheza michezo 30.
City ilianza kuonekana kuwa tishio kubwa kwa Arsenal baada ya kushinda mechi nne mfululizo na kuikaribia kileleni. Hata hivyo, baadaye ilianza kudondosha pointi na kujikuta tena nyuma ya vinara hao.
Sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Nottingham Forest iliharibu kasi yao, na namna Real Madrid ilivyopenya kirahisi katika safu yao ya ulinzi Jumatano inaweza kuwa imepunguza kujiamini kwa wachezaji.
City imeshinda mechi saba zilizopita za Premier League dhidi ya West Ham, lakini itakuwa makini dhidi ya timu inayopambana kubaki kwenye ligi na ambayo inaonyesha dalili za kurejea katika kiwango kizuri.
Kwa upande wa Arsenal, ambayo ilihitaji penalti ya dakika za mwisho kutoka kwa Kai Havertz kupata sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Bayer Leverkusen Jumatano iliyopita, sasa ina nafasi ya kuongeza presha kwa City itakapowakaribisha Everton kwenye mchezo wa leo mapema.
Kikosi cha kocha Mikel Arteta, kinaanza wikiendi kikiwa kileleni kwenye msimamo huku kikiwa kimecheza mechi moja zaidi. Ingawa hivi karibuni kinaonekana kushinda kwa mbinde lakini bado kinapewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua ubingwa msimu huu kikiwa kimebakiza michezo saba tu ili kumaliza ukame wa miaka 22 kwenye klabu hiyo.
Arsenal iko kwenye mfululizo wa ushindi wa mechi tatu za ligi, lakini ushindi wa hivi karibuni dhidi ya Chelsea nyumbani na dhidi ya Brighton & Hove Albion ugenini ulikuwa na presha kubwa huku jitihada za kutafuta ubingwa wa kwanza tangu 2004 zikianza kuonekana kutimia.
Everton imeshinda mara moja tu katika ligi kwenye Uwanja wa Emirates dhidi ya Arsenal (mwaka 2021), lakini safari hii itawasili ikiwa imepumzika vizuri na ikiwa imeshinda mechi mbili mfululizo, huku pia ikiangalia uwezekano wa kufuzu mashindano ya Ulaya kutokana na nafasi iliyopo kwa sasa.
Timu hiyo ipo nafasi ya nane kwenye msimamo na pointi 43, hizi ni aina ya timu ambazo zimekuwa zikiisumbua sana Arsenal msimu huu, hivyo ni mechi yenye presha kubwa kwao.
Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, alipata pigo lake kubwa la kwanza tangu kuchukua nafasi ya Enzo Maresca baada ya timu yake kufungwa mabao 5-2 na Paris Saint‑Germain kwenye UEFA Jumatano.
Chelsea, ambayo ipo nafasi ya tano kwenye msimamo, italazimika kusahau haraka matokeo hayo itakapowakaribisha Newcastle United, ambao walionyesha kiwango bora zaidi miongoni mwa vilabu vya England wiki hii kwa kutoa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya FC Barcelona.
Huu ni mchezo mkubwa ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote leo.
Mabingwa watetezi Liverpool, ambao walipoteza 1-0 dhidi ya Galatasaray Jumanne na kuanzisha mlolongo mbaya wa matokeo kwa vilabu vya England, wako hatarini kumaliza nje ya nafasi tano za juu kwa sasa wakiwa na pointi 48 katika nafasi ya sita kwenye msimamo.
Leo watatakiwa kufanya kazi kubwa wakati watakapovaana na Tottenham Hotspur, ambayo inaendelea kukumbwa na matokeo mabaya na sasa iko kwenye hatari kubwa ya kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu 1977.
Tottenham ilifungwa mabao 5-2 na Atletico Madrid Jumanne, ikiruhusu mabao matatu ndani ya dakika 15 za mwanzo. Hali hiyo imefanya kipindi cha kocha wa muda Igor Tudor kuwa kigumu zaidi, huku beki Micky van de Ven akihofia kile alichokiita “hali ya maafa.”
Kocha huyo raia wa Croatia amepoteza mechi zote nne tangu achukue nafasi ya Thomas Frank, na sasa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilimaliza kwenye nafasi mbaya ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo na pointi 29.