Kansa yatajwa kumuondoa Mutombo
Muktasari:
- Mutombo ambaye anatajwa kuwa mmoja kati wa wazuiaji bora kuwahi kutokea kwenye Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) alifariki akiwa na umri wa miaka 58, huko Atalanta, Marekani.
LEJENDI wa NBA, Dikembe Mutombo, ambaye alifariki jana Jumatatu ameripotiwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na saratani ya ubongo iliyomtesa miaka miwili.
Mutombo ambaye anatajwa kuwa mmoja kati wa wazuiaji bora kuwahi kutokea kwenye Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) alifariki akiwa na umri wa miaka 58, huko Atalanta, Marekani.
Kamishna wa NBA, Adam Silver akizungumzia kifo cha mkongwe huyo alisema: “Dikembe Mutombo alikuwa mkubwa kuliko maisha yake, uwanjani alikuwa mmoja wa wazuia bora na wachezaji wa ulinzi mahiri kuwahi kutokea katika historia ya NBA. Alitumia moyo wake kuwasaidia wengine.”
Mutombo aliyekuwa ana uraia wa DR Congo na Marekani alishawishi wachezaji wengi wa kizazi hiki kuingia kwenye kikapu.
Katika enzi za uchezaji wake alitumikia timu mbalimbali kwa misimu 18 akichezea Denver, Atlanta, Houston, Philadelphia, New York na New Jersey Nets na pia aliingia katika kikosi cha NBA All Star mara nne. Licha ya ubora na rekodi mbalimbali hakuwahi kushinda taji hata moja la NBA katika maisha ya uchezaji.