Kane: Tunataka kumaliza kazi mapema
Muktasari:
- England itavaana na mabingwa watetezi Argentina kwenye mchezo wa nusu fainali ikitafuta nafasi ya kwenda fainali na kusaka ubingwa wao wa kwanza tangu mwaka 1966.
LOS ANGELES, MAREKANI: NAHIODHA Harry Kane amesema kizazi hiki cha England kimefika wakati wa kuandika historia kwa kutwaa ubingwa baada ya kufika hatua za mwisho mara kadhaa bila kubeba kombe.
England itavaana na mabingwa watetezi Argentina kwenye mchezo wa nusu fainali ikitafuta nafasi ya kwenda fainali na kusaka ubingwa wao wa kwanza tangu mwaka 1966.
“Hiki ni kipindi kizuri kwa timu yetu ya taifa, lakini bado tunahitaji kumaliza kazi. Hicho ndicho kipande kinachokosekana,” alisema mshambuliaji huyo wa Bayern Munich. Kane alikiri kuwa England bado haijafikia kiwango chake bora licha ya kufuzu nusu fainali.
“Kocha anajua uwezo tulionao. Anaamini tunaweza kucheza vizuri zaidi na sisi pia tunafahamu bado tuna kiwango kingine cha kuonyesha.”
England sasa itakutana na Argentina katika nusu fainali ya kusisimua itakayopigwa Jumatano, huku mshindi akitinga fainali ya Kombe la Dunia.