Kane aweka rekodi Bayern ikifuzu robo UEFA kwa kishindo
Muktasari:
- Nahodha huyo wa England, alianza mchezo akiwa na mabao 48, lakini penalti ya kipindi cha kwanza na bao la kuvutia kipindi cha pili vilimfikisha jumla ya mabao 50.
HARRY Kane amefikisha mabao 50 katika UEFA Champions League wakati Bayern Munich ilipoifunga Atalanta mabao 4-1 na kufuzu robo fainali.
Nahodha huyo wa England, alianza mchezo akiwa na mabao 48, lakini penalti ya kipindi cha kwanza na bao la kuvutia kipindi cha pili vilimfikisha jumla ya mabao 50.
Kane amefikia rekodi hiyo katika michezo 66, idadi sawa na Lionel Messi na michezo 25 pungufu kuliko Cristiano Ronaldo.
Mchezaji wa Manchester City, Erling Haaland, ndiye anayeshikilia rekodi ya kufikisha mabao 50 kwa haraka zaidi, akifanya hivyo katika michezo 49.
Bayern tayari walikuwa karibu kufuzu kabla ya mechi ya marudiano ya usiku wa Jumatano Machi 18, 2026 baada ya kushinda 6-1 nchini Italia, lakini waliendeleza ushindi mkubwa na sasa inakwenda robo fainali kukabiliana na Real Madrid ikifuzu kwa jumla ya mabao 10-2.
Bao la kwanza lilipatikana dakika ya 25 baada ya Bayern kupewa penalti kufuatia mapitio ya VAR, ambapo Giorgio Scalvini alizuia mpira wa Kane kwa mkono.
Kane alipopiga penalti, shuti lake liliokolewa, lakini mwamuzi akaamuru irudiwe baada ya kipa Marco Sportiello kutoka mstarini mapema.
Safari hii Kane hakukosea, akipiga kwa nguvu huku kipa akiruka upande tofauti.
Hiyo ilikuwa penalti ya 14 aliyofunga msimu huu katika mashindano yote, na ilimfikisha mabao 46 kwa jumla msimu huu.
Kane kisha alifunga bao lake la pili usiku huo na la 50 kwenye mashindano hayo kwa shuti kali lililoenda moja kwa moja juu ya nyavu.
Tayari Kane ndiye Muingereza mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Bayern waliongeza bao la tatu kupitia kijana mwenye umri wa miaka 18, Lennart Karl aliyefunga baada ya pasi ya Luis Díaz.
Díaz naye alikamilisha ushindi kwa kufunga bao la nne baada ya mashambulizi ya kushtukiza, kabla ya Lazar Samardžić kufunga bao la kufutia machozi kwa wageni.