Juventus wajibiwa ishu ya Federico Chiesa
Muktasari:
- Ripoti kutoka Italia zinafichua kwamba uhamisho huo utakamilishwa baada ya kukamilika kwa mashindano ya Afcon 2025. Hilo ni kutokana na Liverpool kuwa na staa wao muhimu Mohamed Salah, anayekipiga kwenye mashindano ya Afcon 2025, akiwa na kikosi cha Misri, kilichotinga hatua ya nusu fainali.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imeripotiwa kuwaambia Juventus ni wakati gani Federico Chiesa atakwenda kuungana nao.
Miamba hiyo ya Serie A inahitaji saini ya mchezaji huyo ikitaka kumng’oa Anfield imrudishe Italia, ambako atakwenda kupata nafasi ya kucheza kila mechi.
Amekuwa na wakati mgumu wa kupata namba chini ya kocha Arne Slot na sasa anajiandaa kwenda Turin huku mabingwa hao wa Ligi Kuu England wakipanga ni lini watamfungulia mlango wa kutokea ili kukamilisha uhamisho huo.
Ripoti kutoka Italia zinafichua kwamba uhamisho huo utakamilishwa baada ya kukamilika kwa mashindano ya Afcon 2025. Hilo ni kutokana na Liverpool kuwa na staa wao muhimu Mohamed Salah, anayekipiga kwenye mashindano ya Afcon 2025, akiwa na kikosi cha Misri, kilichotinga hatua ya nusu fainali.
Kinachoripotiwa ni kwamba Chiesa amekubaliwa uhamisho wake wa kwenda Turin, ambapo sasa mchezaji huyo alilazimisha dili la mkopo, wakati mabosi wa Liverpool wanataka ikiwezekana abebwe tu jumla. Mazungumzo juu ya jambo hilo bado yapo wazi kila upande ukitazama kile ambacho kitakuwa na faida.
Kinachoelezwa ni kwamba wakala wa mshambuliaji huyo anatarajia kwenda Italia, Januari 20 kujadili uhamisho huo. Hadi sasa msimu huu, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amecheza mechi 20 tu katika mashindano yote.
Kutokana na Mo Salah kuwapo kwenye Afcon, huku Alexander Isak akiwa majeruhi, kocha Slot amekuwa akimpa nafasi zaidi Hugo Ekitike kwenye fowadi yake na mara chache akimtumia Chiesa, ambaye ilidhaniwa kwamba kwenye mechi ya jana Jumatatu kwenye Kombe la FA dhidi ya Barnsley angeanzishwa.