Juve isiyoshinda yamvuruga Allegri

Thursday September 23 2021
nga pic

TURIN, ITALIA . UVUMILIVU umefika kikomo. Kocha Mkuu wa Juventus, Massimiliano Allegri hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuwaporomoshea lugha chafu na matusi mastaa wa timu hiyo baada ya kucheza mechi nne mfululizo kwenye Serie A bila kupata ushindi.

AC Milan iliwabana Old Lady na kutoka nao sare ya bao 1-1 Jumapili iliyopita jambo linalofanya kikosi hicho cha Kocha Allegri kushika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Serie A.

Alvaro Morata aliifungia Juventus bao la kuongoza kwa kichwa, lakini Milan ilipambana na kusawazisha dakika za mwisho kwa kichwa pia, bao lililofungwa na Ante Rebic.

Sare hiyo imewafanya mabingwa hao mara 26 wa Italia kuwa na mwanzo mbaya kwenye ligi, wakishindwa kupata matokeo ya ushindi kwenye mechi nne za mwanzo wa msimu tangu mwaka 1961. Kunani Juventus?

Vyombo vya habari za Italia zimeshindwa kuivumilia Juventus.

Magazeti ya michezo Corriere dello Sport lilitoka na kichwa cha habari ‘wanazama’ wakati Tuttosport la Turin liliandika Juve ni ‘majanga’.

Advertisement

Yote yanatokea baada ya klabu hiyo kumpiga bei supastaa wa nguvu Cristiano Ronaldo kwenda Manchester United.

Hilo lina maana Allegri awamu yake ya pili kwenye kiti cha ukocha cha kuinoa miamba hiyo ya Turin imekuwa ngumu kwelikweli tofauti na ilivyokuwa kwenye awamu ya kwanza na alishinda ubingwa wa ligi kwenye misimu yake yote mitano.

Allegri, 54, alirekodiwa na mmoja wa mashabiki wakati akiingia kwenye korida za uwanja wa Allianz baada ya filimbi ya mwisho, video ambayo imepata umaarufu kwelikweli Italia.

Kwenye video hiyo fupi, Allegri alisikika akitoa tusi ‘F***’, kisha akasema “mnachezea Juventus!” wakati akiondoka uwanjani kwa hasira.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Allegri alisema: “Licha ya kipindi cha kwanza kizuri kabisa, kulipotengeneza nafasi nyingi, bado tumeruhusu nafasi moja tu ya Milan na hata tulijiweka kwenye hatari ya kupoteza mechi mwishoni, wakati tulikuwa tumetawala.

“Bahati mbaya tulipoteza umakini, mipango na mapengo. Tazama ile kona ambayo tumeruhusu kufungwa bao, ulikuwa upuuzi mkubwa.

“Haiwezekani kabisa kupoteza hi mechi kwa namna tulivyokuwa tumeitawala. Ukweli, tunahitaji kupiga hatua. Tunahitaji zaidi.”

Wakiwa wamevuna pointi mbili katika mechi nne, Juventus watakuwa na kibarua cha kuwakabili Spezia ugenini leo Jumatano, huku wakiwa na shughuli pevu ya kuwakabili Chelsea kwenye mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Miamba hiyo ya Italia, sasa imecheza mechi 18 mfululizo bila ya kuzuia wavu wake usiguswe, ikiwa ni ishara kwamba wamekuwa na beki nyepesi kuliko yoyote kwenye Ligi Kuu tano bora za Ulaya.

Wamefunga mabao manne tu hadi sasa msimu huu, ikiwamo ni machache kuliko aliyofunga Ronaldo peke yake kwenye kikosi cha Man United tangu alipoachana nao kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Advertisement