Jurgen Klopp anataka timu mbili tu
Muktasari:
- Klopp, mwenye umri wa miaka 58, amekuwa nje ya kazi ya ukocha tangu Mei 2024 baada ya kumaliza safari yake ya miaka tisa iliyojaa mafanikio makubwa katika kikosi cha Liverpool, akitaja uchovu kama sababu ya kuamua kujiweka kando.
MUNICH, UJERUMANI: HABARI ndo hiyo. Jurgen Klopp yuko tayari kurejea kwenye ukocha endapo tu atapata mojawapo ya nafasi mbili; kuinoa Real Madrid au timu ya taifa ya Ujerumani.
Klopp, mwenye umri wa miaka 58, amekuwa nje ya kazi ya ukocha tangu Mei 2024 baada ya kumaliza safari yake ya miaka tisa iliyojaa mafanikio makubwa katika kikosi cha Liverpool, akitaja uchovu kama sababu ya kuamua kujiweka kando.
Kocha huyo Mjerumani baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Soka wa Kimataifa wa Red Bull, Januari 2025, nafasi ambayo inamhusisha na usimamizi wa jumla wa timu zote za soka zilizo chini ya kampuni hiyo.
Klopp, ambaye pia aliwahi kuinoa Borussia Dortmund alidokeza, Juni mwaka jana kuwa huenda safari yake ya ukocha imefikia mwisho, baada ya kukiri kuwa hataki maisha hayo tena.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usajili, Florian Plettenberg, Klopp anaweza kuwa karibu kubadili msimamo wake kabisa. Lakini kuna miradi miwili pekee ambayo inaweza kumshawishi Mjerumani huyo kurejea kwenye msongamano wa maisha ya soka.
Moja ni Real Madrid, klabu ambayo daima imekuwa ikimvutia, na Klopp anafikiria kwa umakini nafasi hiyo iwapo mabingwa wa Ulaya mara 15 watafanya hatua rasmi kuelekea kumchukua majira ya joto yajayo. Chaguo la pili ni timu ya taifa ya Ujerumani, ambayo inajiandaa kushiriki Kombe la Dunia 2026 majira ya kiangazi huko Marekani, Canada na Mexico.
Kocha wa sasa wa Ujerumani, Julian Nagelsmann, atalazimika kujithibitisha baada ya kuchukua nafasi ya Hansi Flick, aliyekuwa kocha wa kwanza kabisa wa Ujerumani kufutwa kazi mwaka 2023. Hata hivyo, chanzo hicho hicho kinasema Klopp yuko na furaha kwenye kibarua chake cha sasa huko Red Bull.
Real Madrid ilimfuta kazi kocha Xabi Alonso kufuatia kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa wapinzani wao Barcelona katika Super Cup ya Hispania Jumapili iliyopota na imemtea kocha wa vijana, Ã lvaro Arbeloa kuongoza timu hiyo.