Jurgen Klopp akanusha uvumi wa kuinoa Real Madrid
Muktasari:
- Kauli hiyo inaonyesha wazi kuwa kwa sasa hayupo karibu kurejea kwenye ukocha wa kiwango cha juu kama wa Madrid. Kwa sasa Klopp anafanya kazi kama mkuu wa soka wa kimataifa ndani ya Red Bull GmbH, akiwa na mkataba unaoendelea hadi 2029.
BERLIN, UJERUMANI: KOCHA wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp amekanusha taarifa za kurejea kufundisha soka zinazomhusisha na Real Madrid, “hazina ukweli wowote.”
Klopp amesema hajawahi kuwa na mawasiliano yoyote na klabu hiyo ya Hispania.
“Habari zote zinazotoka ni upuuzi mtupu. Hawajawahi kunipigia (simu) hata mara moja. Hata wakala wangu hajawahi kupigiwa,” amesema.
Kwa utani, Klopp aliongeza: “Labda ningependa pia kuichukua Atlético Madrid kwa wakati mmoja… samahani Madrid, mtalazimika kupiga simu kwanza.”
Kauli hiyo inaonyesha wazi kuwa kwa sasa hayupo karibu kurejea kwenye ukocha wa kiwango cha juu kama wa Madrid. Kwa sasa Klopp anafanya kazi kama mkuu wa soka wa kimataifa ndani ya Red Bull GmbH, akiwa na mkataba unaoendelea hadi 2029.
Hata hivyo, Klopp aliacha mlango wazi kwa uwezekano wa kurejea kufundisha siku zijazo.
“Kwa umri wangu maisha yanaendelea vizuri, lakini kama kocha bado sijamaliza kabisa (kufundisha). Sijafikia umri wa kustaafu. Nani anajua kitakachotokea miaka ijayo? Lakini kwa sasa hakuna mpango wowote,” amesema.
Kauli yake inaashiria kuwa ingawa kwa sasa hayupo tayari kurudi benchi, bado anaweza kufanya hivyo baadaye.
Klopp pia alikanusha uvumi wa kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani, akisema hafikirii kuhusu hilo kwa sasa.
Kwa sasa, kocha huyo anaonekana kuridhika na nafasi yake ndani ya mfumo wa Red Bull, akihusika zaidi na mipango ya kimkakati badala ya majukumu ya kila siku ya ukocha.
Ingawa jina lake litaendelea kuhusishwa na klabu kubwa Ulaya kutokana na historia na mafanikio yake, msimamo wake uko wazi, “hakuna mawasiliano, hakuna mpango wa haraka wa kurejea kufundisha, angalau kwa sasa.”