Kuhusu Madrid, Klopp ukweli ni huu
Muktasari:
- Ingawa kwa sasa anafanya kazi kama mkuu wa masuala ya soka katika Kampuni ya Red Bull GmbH inayomiliki klabu mbalimbali barani Ulaya, uvumi kutoka Hispania umeeleza kocha huyo aliyewahi kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya ni miongoni mwa majina yanayotazamwa na vigogo wa Madrid wanaoendelea kutafuta kocha wa kudumu.
MADRID, HISPANIA: MUSTAKABALI wa Kocha Jurgen Klopp kwa mara nyingine umeanza kuzua mjadala mkubwa baada ya ripoti mbalimbali kudai anafikiria kurejea tena kwenye benchi la ufundi baada ya kupewa ofa ya ajira na Real Madrid.
Ingawa kwa sasa anafanya kazi kama mkuu wa masuala ya soka katika Kampuni ya Red Bull GmbH inayomiliki klabu mbalimbali barani Ulaya, uvumi kutoka Hispania umeeleza kocha huyo aliyewahi kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya ni miongoni mwa majina yanayotazamwa na vigogo wa Madrid wanaoendelea kutafuta kocha wa kudumu.
Klopp alihusishwa na nafasi ya ukocha katika klabu ya Madrid kwa muda mrefu, huku taarifa zikidai mabingwa hao wa Hispania wanamwona Mjerumani kama mtu atakayeleta utulivu katika klabu hiyo.
Hata hivyo, wakala wake wa muda mrefu Marc Kosicke amezungumzia hilo, akisisitiza mteja wake hana mpango wa kufundisha timu yoyote kwa sasa.
Akizungumza kuhusu uvumi unaoendelea kuenea, Kosicke alisema: "Hakuna haja ya kujibu maswali kuhusu mambo ambayo ni uvumi tu. Hakuna mtu ambaye amewasiliana na sisi hadi sasa. Jurgen Klopp ana furaha sana na nafasi yake ya sasa Red Bull GmbH, na kile kinachosemwa kuhusu mazungumzo ya kuifundisha Real Madrid ni uvumi tu kwa sasa.”
Kauli hiyo imekuja wakati na ripoti nyingine zikidai kuwa pia Atletico Madrid pia ilikuwa ikimfuatilia Klopp ili akawe mrithi wa Diego Simeone.
Ingawa Simeone bado ana mkataba hadi mwaka 2027, baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa viongozi wa Atletico wanafikiria uwezekano wa kufanya mabadiliko baadaye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Red Bull Oliver Mintzlaff pia amekanusha vikali madai Klopp anataka kuondoka.