Julian Nagelsmann afunguka kiwango cha Wirtz
Muktasari:
- Wirtz, mwenye umri wa miaka 22, alijiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni 116 milioni dirisha lililopita la majira ya kiangazi na alikataa ofa ya Bayern Munich.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot, ametumiwa ujumbe na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann ambaye amesema kiwango kisichoridhisha kinachoonyeshwa na Florian Wirtz si kosa la staa huyo.
Wirtz, mwenye umri wa miaka 22, alijiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni 116 milioni dirisha lililopita la majira ya kiangazi na alikataa ofa ya Bayern Munich.
Manchester City na Real Madrid pia zilikuwa zinavutiwa na kiungo huyo, aliyeonyesha kiwango bora akiwa na Bayer Leverkusen.
Wirtz alianza vyema katika kikosi cha Liverpool akitoa asisti katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Crystal Palace, lakini katika michezo 12 iliyofuata ya michuano yote akiwa na klabu na timu ya taifa, ametoa asisti moja.
Wirtz hakufunga wala kutoa asisti katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Luxembourg Ijumaa, lakini alicheza vizuri katika eneo la kiungo kiasi cha kuwapoteza kabisa viungo wa timu pinzani.
Baada ya mchezo kocha Nagelsmann alimpongeza Wirtz na kumtetea kutokana na hali yake ya kutokufunga akisema:
“Hata kama hajafunga bao, yeye ndiye mchezaji anayetengeneza nafasi nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England. Si kosa lake kama wachezaji wenzake hawazitumii nafasi hizo kufunga mabao, licha ya kufanya hivyo, pia tusisahau huyu ni mchezaji mpya, anahitaji kuzoea kwanza.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu rasmi za Ligi Kuu England, zinapingana na kauli za Nagelsmann kwani zinaonyesha Wirtz hayuko hata kwenye nafasi tano za juu za wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi msimu huu.
Baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakimkosoa sana staa huyu na kutaka asipangwe katika kikos cha kwanza kwani kiwango chake ndio kinasababisha Liverpool isicheze vizuri.
Mchambuzi na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Jamie Carragher, aliwahi kusema:”Kwa sasa, sipendi timu inavyocheza kuna mtu kama Florian Wirtz hafai kuanza kwa sababu hana hata kasi. Naelewa ni mchezaji mpya, anahitaji kujifunza lakini kwa sasa hafai kuanza katika timu.”