Jude Bellingham apewa ujanja Real Madrid

Muktasari:
- Staa huyo alikuwa na msimu uliopita wa majanga mengi huko Bernabeu wakati Los Blancos ilipotoka patupu bila kubeba taji lolote kwa mara ya kwanza katika misimu minne ya mwisho.
MADRID, HISPANIA: KIUNGO Jude Bellingham amepewa ujanja kuhakikisha anarudi kwenye ubora wake kwa haraka kwa sababu kocha mpya wa Real Madrid, Xabi Alonso anaweza kumchezesha kwenye nafasi anayotaka.
Staa huyo alikuwa na msimu uliopita wa majanga mengi huko Bernabeu wakati Los Blancos ilipotoka patupu bila kubeba taji lolote kwa mara ya kwanza katika misimu minne ya mwisho.
Msimu wake wa kwanza Bellingham alikuwa moto uwanjani, kabla ya mambo kugeuka kwenye msimu wa pili na kujikuta akikosolewa vikali kwenye vyombo vya habari vya Madrid.
Winga wa zamani wa Real Madrid, Victor Sanchez del Amo anaamini kiungo huyo hakuwa na wakati mzuri msimu uliopita kwa sababu hakuwa akichezeshwa kwenye nafasi inayomfanya acheze kwa ubora wake.
Bellingham, 21, ana matumaini makubwa atarudi kwenye ubora wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani, ambapo Real Madrid itacheza mechi yae ya kwanza dhidi ya Al-Hilal huko Miami, Jumatano.
Sanchez del Amo, 49, alisema: “Niliona badiliko kubwa sana kwa Bellingham kwenye msimu wa pili.
“Msimu wa kwanza alikuwa bora uwanjani, alicheza kwenye nafasi ya ubora wake kwa maana ya kuwa huru katika kiungo ya kati. Lakini, msimu uliopita, alikuwa akichezeshwa kiungo kwenye upande wa kushoto.
“Alikuwa na majukumu tofauti ya kiufundi na hilo halikuwa likimfurahisha. Real Madrid ilipoteza Toni Kroos na haikuziba pengo lake, hivyo iliwafanya washindwe kuwa na muunganiko kati ya safu ya ulinzi na ushambuliaji.
“Bellingham aliona hilo na kujaribu kusaidia timu kwa kushuka chini, kitu ambacho kilimfanya asiwe kwenye ubora wake. Unaweza kuona lugha ya ishara kwa muda wote aliokuwa uwanjani ndiyo maana alikuwa akilalamika sana, kuonyesha kadi za njano kutokana kulumbana na wachezaji wa upinzani uwanjani.”
Bellingham amechelewesha upasuaji wa bega ili amalizane na fainali za Kombe la Dunia la Klabu kwanza, ambapo kikosi cha timu yake kimepanga kuchuana na Al-Hilal,Pachuca na RB Salzburg kwenye makundi.
Madrid itakuwa chini ya kocha mpya Alonso, aliyetua kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti, aliyetimkia kuinoa timu ya taifa ya Brazil mwishoni mwa msimu uliopita.