Johan Manzambi apagawisha vigogo
Muktasari:
- Baada ya kufanikisha ndoto hiyo, hakutosheka kwa kuitwa kikosini pekee, bali aliamua kutumia fursa hiyo kuonyesha uwezo wake na kuwa mmoja wa wachezaji waliotikisa zaidi mashindano hayo.
ZURICH, USWISI: KIUNGO chipukizi wa Uswisi, Johan Manzambi, ameendelea kuthibitisha kuwa ni mmoja wa nyota wanaochipukia kwa kasi katika soka la dunia baada ya kung'ara katika Kombe la Dunia 2026 na kujiweka kwenye rada ya klabu kadhaa kubwa za Ulaya.
Kwa Manzambi, kucheza Kombe la Dunia haikuwa ndoto ya ghafla. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 alikuwa amejiwekea lengo la kushiriki mashindano hayo hata kabla hajacheza mechi yake ya kwanza akiwa Freiburg au kuitwa katika kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya Uswisi.
Baada ya kufanikisha ndoto hiyo, hakutosheka kwa kuitwa kikosini pekee, bali aliamua kutumia fursa hiyo kuonyesha uwezo wake na kuwa mmoja wa wachezaji waliotikisa zaidi mashindano hayo.
Kocha wa Uswisi, Murat Yakin, alilazimika kumpa nafasi ya kuanza kikosini baada ya Manzambi kuingia akitokea benchi na kufunga mabao mawili dhidi ya Bosnia na Herzegovina katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi.
Kiungo huyo aliendelea kuonyesha kiwango bora kwa kufunga bao moja na kutoa asisti moja katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia aliyoanza dhidi ya Canada, kabla ya kutoa pasi ya bao katika ushindi dhidi ya Algeria kwenye hatua ya 32 bora.
Hata hivyo, Manzambi alikosa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Colombia kutokana na majeraha ya goti, na bado haijafahamika kama atakuwa fiti kuikabili Argentina katika robo fainali.
Licha ya changamoto hiyo, tayari ameweka rekodi baada ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mchango wa mabao matano (kufunga na kutoa asisti) katika Kombe la Dunia tangu takwimu hizo zilipoanza kurekodiwa mwaka 1966.
Rafiki yake wa karibu, Yann Sturm, anaamini mafanikio hayo ni mwanzo tu wa safari kubwa.
"Nina uhakika tutasikia mengi zaidi kuhusu Johan katika miaka ijayo," amesema Sturm.
Nyota aliyepania mafanikio
Kupanda kwa kasi kwa Manzambi hakujatokea kwa bahati mbaya.
Baada ya kuhamia Freiburg akitokea Servette mwaka 2023, ari yake ya kujifunza na kujiendeleza iliwavutia makocha wa klabu hiyo.
Kocha wa zamani wa Freiburg II, Benedetto Muzzicato, alikumbuka tukio ambalo lilionyesha namna kiungo huyo alivyo na kiu ya maendeleo.
Baada ya mazoezi marefu ya kikosi cha pili, Manzambi alimfuata kocha huyo na kuomba wapitie tena mpango wa mchezo kwa sababu alihisi bado hakuwa ameuelewa ipasavyo.
"Anataka kuwa bora kila siku. Wakati mwingine kazi yetu huwa si kumhamasisha, bali kumzuia asijifunze kupita kiasi," amesema Muzzicato.
Ameongeza kuwa tabia hiyo ndiyo iliyomfanya Manzambi aanze kuvutia klabu mbalimbali hata kabla ya Kombe la Dunia kuanza.