JIWE LA SIKU: Kinachoweza kutokea vita ya ubingwa Ligi Kuu England

Muktasari:

  • Hata hivyo, mbio hizo za ubingwa hazijafika tamati kwa kuwa Liverpool na Arsenal bado zina mechi sita za kucheza, sawa na pointi 18, huku msimamo unavyosoma tofauti ni pointi mbili tu.

LONDON, ENGLAND: Baada ya wikiendi iliyopita, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England zilihamia kwenye mikono ya Manchester City.

Hata hivyo, mbio hizo za ubingwa hazijafika tamati kwa kuwa Liverpool na Arsenal bado zina mechi sita za kucheza, sawa na pointi 18, huku msimamo unavyosoma tofauti ni pointi mbili tu.

MSIMAMO ULIVYO 2023/24

                                P             GD          Pts

1.Man City          32           +44         73

2.Arsenal             32           +49         71

3.Liverpool          32           +41         71


Bado kuna mambo mengi yanayoweza kutokea. Kilichoshtua ni baada ya kuona Man City ikishinda Jumamosi kwa ushindi mzito, kabla ya wapinzani wake kwenye mbio hizo za ubingwa, Liverpool na Arsenal zote kupoteza mechi zao walizocheza nyumbani Anfield na Emirates mtawalia, Jumapili.

Man City iliingia uwanjani Jumamosi ikiwa kwenye nafasi ya tatu, lakini baada ya wikiendi hiyo kupita, ilijikuta kileleni kwenye msimamo huo na kuziacha kwenye mataa Arsenal na Liverpool baada ya kuangusha pointi.

Hata hivyo, kiungo wa zamani wa Ligi Kuu England, Owen Hargreaves alisema mbio za ubingwa huo wa Ligi Kuu England hazijakwisha, kwani kuna uwezekano mkubwa Man City nayo itaangusha pointi kabla ya kufika mwisho.

Vita ya ubingwa wa Ligi Kuu England imekuwa tamu kinoma. Ni mara moja tu, msimu wa 2013/14, ndiyo ulioshuhudia timu tatu zikichuana vikali kwenye kusaka ubingwa na mchakamchaka wake ulikuwa mkali, baada ya mechi 32, timu tatu za juu zilikuwa zimetofautiana pointi tatu tu, ukilinganisha na sasa pointi mbili.


MBIO ZA UBINGWA 2013/14

                                P             GD          Pts

1.Man City          38           +65         86

2.Liverpool          38           +51         84

3.Chelsea            38           +44         82

Msimu wa 2013/14 vita ilikuwa hadi kwenye wiki chache za mwishoni na tukio linalokumbukwa ni lile la Steven Gerrard kuanguka wakati Liverpool ilipochapwa 2-0 na wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa Chelsea.

Kutokana na hilo bado inasubiriwa kuona kama kwenye mechi sita ilizobakiza kila timu kama kutakuwa na tukio litakaloleta athari kwenye matokeo ya kunogesha zaidi vita huyo ya kufukuzia ubingwa wa ligi.


SIKU ILIZOTUMIKIA ZILIZOKAA

KILELENI KWENYE MSIMAMO 2023/24

Liverpool             87

Man City              68

Arsenal                 53

Spurs                     26

Brighton               7

Newcastle           7

West Ham           2


Kinachovutia ni mara nane kwenye historia ya Ligi Kuu England, timu iliyokuwa kileleni kwenye msimamo baada ya mechi 32, ilikwenda kunyakua ubingwa.


BINGWA AMBAYE HAKUWA KILELENI

KWENYE MSIMAMO KATIKA MECHI YA 32

1997/98                Arsenal                 2

1998/99                Man Utd                2

2002/03                Man Utd                 2

2009/10                Chelsea                  2

2011/12                Man City                  2

2013/14                Man City              3

2018/19                Man City              2

2022/23                Man City              2


Man City haitishi kuzidi Liverpool

Rekodi zinaonyesha Liverpool ndiyo timu iliyovuna pointi nyingi zaidi kwenye mechi sita za mwisho kwa kulinganisha na Man City.

Namba zinasoma, kikosi hicho cha Jurgen Klopp kimevuna pointi 77 katika mechi sita za mwisho za msimu katika kipindi cha misimu mitano iliyopita, wakati Guardiola amevuna pointi 73.

Rekodi za Guardiola v Klopp kwenye mechi sita za mwisho

                                               Guardiola            Klopp

Msimu                                   W-D-L   Pts          W-D-L   Pts

2018/19                                6-0-0      18           6-0-0      18

2019/20                                5-0-1      15           4-1-1      13

2020/21                                4-0-2      12           5-1-0      16

2021/22                                5-0-1      15           5-1-0      16

2022/23                                4-1-1      13           4-2-0      14

Jumla                                      24-1-5   73           24-5-1   77


Lakini, kinachoweka ubora wa Man City kwenye hili ni kwamba imebeba ubingwa mara mbili kwa staili hiyo, wakati Liverpool imebeba mara moja.

Arsenal mara kadhaa imekuwa kwenye mbio za ubingwa, lakini haijawahi kuwa kwenye ubora mkubwa katika mechi sita za mwisho na rekodi yao tamu ni ya msimu ulipita na kwenye mechi sita za mwisho, ilivuna pointi tisa tu, ikishinda tatu na kupoteza tatu.

Kwa maana hiyo, hicho ndicho kitu kinachotoa imani kubwa kuna kitu kinaweza kutokea hadi kufikia mwisho wa msimu huu wa 2023/24.

Mechi zilizobaki

Man City inakabiliwa na wapinzani wasumbufu kwelikweli kwenye mechi zao sita zilizobaki. Kwanza wataanzia ugenini kukipiga na Brighton, kisha itatoka tena kwenda kukipiga na Nottingham Forest kabla ya kurudi nyumbani kucheza na Wolves.

Itatoka tena kwenda ugenini kuzikabili Fulham na Tottenham kabla ya kurudi nyumbani kumaliza msimu kwa kumenyana na West Ham United.

Kwenye karatasi, Man City haionekani kuwa na ratiba ngumu sana, lakini ndani ya uwanja mambo yanaweza kuwa tofauti hasa wachezaji wanavyoonyesha kuchoka.

Liverpool inaonekana kuwa na tatizo kwenye safu yake ya ulinzi. Miamba hiyo imeshinda mechi mbili tu kati ya tano za mwisho kwenye Ligi Kuu England na mechi tatu kati ya nane ilizocheza kwenye michuano yote, imesukumwa nje kwenye Kombe la FA na Europa League ndani ya muda huo.

Shida ya Liverpool kwa sasa ni kwamba haifungi mabao huku yenyewe ikiruhusu nyavu zao kuguswa kirahisi.

Ratiba yao, watakipiga na Fulham ugenini, kisha itatoka tena kucheza na West Ham kabla ya kurudi nyumbani kucheza na Tottenham na watatoka kucheza na West Ham ba Aston Villa kabla ya kurudi Anfield kucheza na Wolves.

Kasheshe la Arsenal ni ina mechi tatu ngumu za ugenini. Kipute cha kwanza watakuwa ugenini kukabilisha na Wolves baada ya hapo itarudi nyumbani Emirates kucheza na Chelsea, kabla ya kutoka tena kwenda ugenini kwenye North London derby kuwakabili Tottenham.

Watarudi nyumbani kucheza na Bournemouth, kabla ya kwenda ugenini kucheza na Manchester United na kumaliza msimu wao nyumbani kukabiliana na Everton.


MATOKEO YA ARSENAL YA UGENINI

KWENYE MECHI 11 ZILIZOPITA

Lens                                       2-1 (Imepoteza)

Chelsea                                                2-2 (Sare)

Sevilla (UCL)                       1-2 (Imeshinda)

West Ham (EFL Cup)       3-1 (Imepoteza)

Newcastle                           1-0 (Imepoteza)

Brentford                            0-1 (Imeshinda)

Luton Town                        3-4 (Imeshinda)

Aston Villa                           1-0 (Imepoteza)

PSV Eindhoven (UCL)     1-1 (Sare)

Liverpool                             1-1 (Sare)

Fulham                                 2-1 (Imepoteza)