Salah, Klopp ugomvi kawaida yao

Muktasari:

  • Hata hivyo, historia inaonyesha wawili hawa wamewahi kuingia kwenye sintofahamu mara kadhaa wakati ambao Salah anaambiwa atoke uwanjani.

LIVERPOOL ENGLAND: Hivi karibuni moja kati ya matukio yaliyoongelewa sana ni kitendo cha staa wa Liverpool, Mohamed Salah kubishana na kocha wake Jurgen Klopp wakati anafanyiwa mabadiliko ya kuingia uwanjani katika mchezo dhidi ya West Ham.

Hata hivyo, historia inaonyesha wawili hawa wamewahi kuingia kwenye sintofahamu mara kadhaa wakati ambao Salah anaambiwa atoke uwanjani.

Hapa tumekuletea matukio matano ya Salah na Klopp kugombana wakati staa huyo anafanyiwa mabadiliko ya kutolewa ama kuingizwa uwanjani, ukijumlisha na hilo la West Ham.


Sheffield United vs Liverpool Aprili 2024

Dakika mbili tangu Sheffield United iliposawazisha Klopp aliamua kumfanyia mabadiliko Mohamed Salah na wakati anatoka alimpa mkono Klopp huku akiwa hamuangalii huku usoni akionekana kuwa ni mtu mwenye hasira.

Alitembea na kwenda kwenye benchi la Liverpool bila ya kumuongelesha mtu yeyote. Hata hivyo, mabadiliko yake yalizaa matunda kwani Liveprool ilishinda mabao 3-1.

Chelsea vs Liverpool, Agosti 2023

Mechi ilikuwa ni sare na mizani imebalansi lakini Liverpool ilikuwa inahitaji bao la ushindi katika dakika 10 za mwisho ambapo mchezo ndio ulikuwa umefikia.

Klopp akaamua kumtoa Salah ambaye alishafunga bao lakini lilikataliwa na VAR, nafasi ya Salah akanyanyuliwa  Harvey Elliott.

Baada ya kuona kibao kwamba ni yeye ndiye anayetakiwa kutoka Salah alijifungua plasta iliyokuwa mkononi na kuitupa chini kwa hasira kisha wakati anatoka alikataa kumpa mkono Elliott.

Brighton vs Liverpool Machi 2022

Wakati huu ilikuwa ni Klopp ambaye alionekana kuchafukwa, kocha huyu wa zamani wa Borussia Dortmund alionekana akimfokea Salah baada ya kukosa bao la wazi katika mchezo dhidi ya Brighton.

Salah alikosa baada ya shuti lake kudakwa na Robert Sanchez na Klopp alikuwa akifoka kwa sababu kabla ya Salah kupiga shuti hilo alikuwa na uwezo wa kumpasia Luis Diaz aliyekuwa kwenye eneo zuri zaidi yake. Klopp alirusha mikono juu kwa hasira huku akiongea baada ya Salah kukosa bao hilo.

Brighton vs Liverpool, Novemba 2020

Baada ya kibao kunyanyuliwa na kuonyesha Salah ndiye aliyetakiwa kutoka uwanjani na nafasi yake ichukuliwe na Sadio Mane, alinyoosha mikono juu ishara ya kutoridhishwa na uamuzi uliofanyika.

Wakati anatoka pia alikuwa ni mwenye hasira na hakutaka kuzungumza na mtu yeyote.

Hata hivyo, kutoka kwa Salah ni kama kulizidisha hatari kwenye lango la Liverpool na dakika za jioni Brighton ilipata penalti na kusawazisha hali iliyosababisha mchezo umalizike kwa sare ya 1-1.

Baada ya mechi Klopp alisema: “Siku ambayo Mohamed Salah atafanyiwa mabadiliko kisha akawa anafurahia wakati anatoka basi ujue kutakuwa kuna shida mahali, namuelewa anapokuwa vile lakini kama leo ni kwa sababu hakufanya mazoezi na timu kwa muda kwani alikuwa akiumwa Covid 19, alicheza dakika 60 mechi iliyopita na akapumzika siku tatu ambapo leo amecheza tena, tulifanya vile kwa uangalifu najua anachukia lakini hiyo ilikuwa kwa usalama wake.

West Ham vs Liverpool, Aprili 27, 2024

Hii ilikuwa ni hivi juzi wakati anaingizwa uwanjani katika dakika za mwishoni kipindi cha pili, alimpa mkono Klopp na baada ya muda wakaonekana kuzozana.

Straika Darwin Nunez ndio alisimama katikati yao akijaribu kumzuia Salah asimsogelee kocha.

Baada ya mechi alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya hilo Salah alisema akiongea “moto utawaka.”

Kwa upande wa Klopp yeye akasema ameshamalizana na staa huyo na kila kitu kipo sawa kwa sasa.

Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 2-2 iliyowavurugia Liverpool mbio za ubingwa.