Jina la Nunez lapenya Barca

Muktasari:

  • Miamba hiyo ya Nou Camp mpango wao ni kufanya maboresho kwenye kikosi chao kwa maana ya kufanya usajili mkubwa katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku straika Nunez akitazamwa kama mtu mwafaka wa kwenda kuchukua mikoba ya supastaa Robert Lewandowski, ambaye anaweza kuwa mmoja kati ya watakaofunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu.

 BARCELONA, HISPANIA: Jina la straika wa Liverpool, Darwin Nunez limeshtua wengi baada ya kuwekwa kwenye orodha ya wachezaji wanaotazamiwa kwenda kufanya mapinduzi makubwa huko Barcelona msimu ujao.

Miamba hiyo ya Nou Camp mpango wao ni kufanya maboresho kwenye kikosi chao kwa maana ya kufanya usajili mkubwa katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku straika Nunez akitazamwa kama mtu mwafaka wa kwenda kuchukua mikoba ya supastaa Robert Lewandowski, ambaye anaweza kuwa mmoja kati ya watakaofunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu.

Kiwango cha mwisho cha mishahara huko Barcelona kimetajwa kuwa hakizidi sana Pauni 174 milioni, hivyo itawalazimu kuuza baadhi ya masupastaa wao ili kujijenga upya. Kutokana na kupokea mshahara wa Pauni 27 milioni kwa mwaka, Lewandowski ni moja ya wachezaji wenye majina makubwa huko Nou Camp ambao wataondolewa ili kupunguza bajeti ya mishahara.

Nunez ni mmoja wa wachezaji wanaolipwa vizuri huko Liverpool, lakini kiwango anacholipwa ni kama robo tu ya kile ambacho Lewandowski anapokea huko Barcelona.

Kuna wachezaji wengine kadhaa watafunguliwa mlango wa kutokea Nou Camp mwishoni mwa msimu huu, jambo linalowapa uhakika mabosi ni kwamba wataweza kumudu kunasa huduma ya Nunez.