Jeuri ya pesa! Wasaudia wataka Messi akacheze na Ronaldo

RIYADH, SAUDI ARABIA. LISEMWALO lipo, kama halipo laja... Ndivyo inavyosemwa na wengi kuhusu ishu ya nyota wa kimataifa wa Argentina na klabu ya PSG ya Ufaransa, Lionel Messi anayetajwa kutakiwa na moja ya klabu za nchini Saudi Arabia.

Hadi sasa hakuna mwafaka uliofikiwa baina ya mchindi huyo wa Kombe la Dunia na mabosi wa PSG juu ya kuongeza mkataba mpya na awali ripoti zilidai Messi atakuwa tayari kusalia klabuni hapo.

Hata hivyo, kumezuka habari zinazomhusisha nyota huyo na klabu moja kubwa ya Saudi Arabia, Al Hilal na imepanga kumpa mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona mshahara wa Pauni 194 (Sh547 bilioni) kwa mwaka ikiwa ni majumuisho ya mshahara na haki za kutumia taswira yake ikiwa atakubali kujiunga nao. Inaelezwa mshahara huo ni sawa na anaolipwa Cristiano Ronaldo na Al Nassr.

Mapema wiki hii baba mzazi wa nyota huyo, Jorge Messi alionekana kwenye uwanja wa ndege wa Riyadh, Saudi Arabia na taarifa kutoka tovuti mbali mbali barani Ulaya zikaeleza alikuwa ameenda kufanya mazungumzo na mabosi wa moja ya timu nchini humo ili Messi ajiunge nao mara baada ya mkataba wake wa sasa na PSG kumalizika  mwisho wa msimu huu.

Inaelezwa Al Hilal ambao ni wapinzani wakubwa wa Al Nassr timu anayochezea Ronaldo, kwa sasa imetenga kiasi hicho cha pesa ambacho kinaweza kubadilisha upepo na kumfanya Messi atue nchini humo kwenye dirisha lijalo.

Jorge alionekana akiwa kwenye kikao na Profesa Abdullah Hammad, mkuu wa Mahd Sports Academy pamoja na mtu wa karibu wa waziri wa michezo wa nchi hiyo, Prince Abdulaziz Al-Faisal.

Mbali na kutua timu hiyo, mamlaka za nchini humo zinatamani nyota huyo acheze kwenye ligi yao ili kuiongezea thamani kwa uwepo wa ushindani wa wawili hao (Messi na Ronaldo).

Al Nassr na Al Hilal ni mahasimu wa jadi na baada ya Al Nassr kuonyesha jeuri ya fedha kwa Ronaldo wao wanataka kuonyesha jeuri ya fedha kwa Messi.

Awali Messi alionekana kuwa na nafasi kubwa ya kujiunga na timu za Marekani ikiwa majadiliano yake na mkataba na vigogo wa PSG hayatofikiwa mwafaka.

A Hilal ambayo kwa sasa imefungiwa kufanya usajili wowote na FIFA italazimika kusubiri hadi mwisho wa msimu huu na ripoti zinadai serikali imepanga kuondoka ukomo wa timu kulipa mishahara ili kuzipa nafasi timu nyingine pia kufanya usajili wa mastaa mbalimbali wakubwa barani Ulaya.

Kiasi cha pesa mbacho kinatajwa kuwekwa mezani ni ngumu kwa Messi kukipata sehemu yoyote kwa sasa na kutokana na umri wake unazidi kumtupa mkono, taarifa zinaeleza fundi huyo ana zaidi ya asilimia 70 za kutua kwa waarabu hao.

Mbali ya shughuli za usajili, baba yake Messi anadaiwa kuwa nchini humo kwa sababu ya mazungumzo na serikali kwani Messi ni balozi wa utalii wa nchi hiyo.

Messi ambaye alifanya vizuri sana kwa mwaka jana akifanikiwa kuiwezesha Argentina kuchukua Kombe la Dunia, msimu huu amcheza mechi 31 za michuano yote na kufunga mabao 18 na kutoa asisti 17.