Jeremy Doku awapagawisha makocha
Muktasari:
- Pep Guardiola aliiongoza Man City akisherehekea mechi yake ya 1,000 tangu aanze ukocha na kitu kizuri timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool uwanjani Etihad.
MANCHESTER, ENGLAND: KIWANGO bora cha Jeremy Doku wa Manchester City kwenye mechi ya Liverpool kimewakosha makocha wa timu zote mbili na kummwagia sifa kwa kile alichofanya uwanjani.
Pep Guardiola aliiongoza Man City akisherehekea mechi yake ya 1,000 tangu aanze ukocha na kitu kizuri timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool uwanjani Etihad.
Doku alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi kutokana na uwezo wake na hivyo kuisaidia timu yake kupunguza pengo la pointi katika kuwakimbizia vinara Arsenal.
Doku, alifunga bao lake la tatu katika mechi 100 alizochezea Man City na jambo hilo lilimkosha kocha Guardiola, ambaye alimsajili mchezaji huyo kutoka Rennes ya Ufaransa.
“Kucheza nyumbani na kushinda mechi wakati wa kuelekea mapumziko ya mechi ya kimataifa ni kitu kizuri. Gigi (Donnarumma) naye alifanya sevu nzuri. Mabeki wa pembeni wote walikuwa vizuri. Viungo walipiga pasi nyingi sana na kumiliki mchezo. Bila shaka, Jeremy (Doku) alikuwa tishio sana sambamba na Erling (Haaland).”
Alipoulizwa kama Doku alikuwa kwenye kiwango bora kabisa kuwahi kutokea Man City, Guardiola amesema: “Mmoja wa watu bora kabisa hadi sasa. Beki wao wa kulia Conor (Bradley) ni mwepesi, niliona jinsi alivyokabana na Vinicius Junior (vs Real Madrid). Lakini, hapa alikuwa na mechi nzuri.”
Kocha wa Liverpool, Slot naye amesema kitu kuhusu Doku, ambaye alipiga mashuti matatu kulenga goli, huku akishinda vita ya ana kwa ana mara 11 na alipiga pasi 14 katika eneo la Liverpool, ambao walionekana kuwa kwenye kiwango cha hovyo katika mechi hiyo ya Jumapili.
”Kuna lile bao matata kabisa la Doku, alitufanya tuwe 3-0. Lakini, pia niliona timu iliyocheza ikihitaji kushinda.”