Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pep Guardiola kuondoka Manchester City

Pep Pict
Pep Pict

Muktasari:

  • Man City jana ilicheza dhidi ya watani zao wa jadi, Manchester United na kabla ya mchezo huo ilikuwa imeshinda mechi moja tu kati ya 10 za mwisho, ikishika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England nyuma ya Nottingham Forest. 

MANCHESTER, ENGLAND: KAKUBALI yaishe. Ndiyo, Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema anasikilizia matokeo ya mechi katika mwezi mmoja ujao na kama mambo hayataenda vizuri hana budi kung'atuka.

Man City jana ilicheza dhidi ya watani zao wa jadi, Manchester United na kabla ya mchezo huo ilikuwa imeshinda mechi moja tu kati ya 10 za mwisho, ikishika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England nyuma ya Nottingham Forest. 

Mwezi ujao timu yake itakuwa na mechi dhidi ya Man United, Aston Villa, Everton, Leicester, West Ham, Salford City, na Brentford. 

Mbali ya kusema ataondoka ikiwa atafanya vibaya katika mechi hizo, Pep alisema ataondoka endapo wachezaji hawatafuata kile anachosema kwa kupoteza ushawishi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo licha ya kuwa na mkataba unaomalizika mwaka 2027.

"Ni wakati gani nitajua naondoka? Ikiwa nitaendelea kupoteza kwa mwezi ujao, ikiwa hivyo nitasema jamani nafikiria aje mtu mwingine kuikomboa timu na hii hali, kwa sababu haitakiwi kukaa kwa muda mrefu, pia nitaondoka wakati ambao nitaona wachezaji hawafuatishi kile ninachowaambia na hawakimbii tena," alisema Guardiola.

"Ikifikia wakati huo, hamtoweza kuniona hapa naongea na nyinyi hata kwa dakika moja, lakini zaidi ya hapo nitaendelea kuwepo, hakuna shaka kuhusu hilo. Tumeshapata mafanikio hapo awali na tumewahi kuwa bora, hali yetu inanifanya kutambua jinsi ilivyokuwa ngumu kufikia mafanikio tuliyonayo sasa, ikiwa tutapambana na hali hii na kukaa sawa, hatutoweza kusahau nyakati hizi, kwa sababu ni kipindi kigumu sana."

Guardiola amekuwa chini ya shinikizo la kufukuzwa katika wiki za hivi karibuni timu yake ikikumbana na mfululizo wa mechi saba bila ushindi na ni kipindi kibaya zaidi katika kazi yake ya ukocha.

Mechi yao ya mwisho kushinda ilikuwa ni dhidi ya Nottingham na ilipata mabao 3-0 yaliyofungwa na Bernardo Silva, Kevin De Bruyne na Jeremy Doku.

Man City ilishinda taji la Ligi Kuu England mara nne mfululizo ikichukua kwa tofauti ya alama tatu dhidi ya Arsenal msimu uliopita, msimu huu ina tofauti ya alama tisa dhidi ya vinara vijana wa Arne Slot, Liverpool ambao wamekuwa katika kiwango bora na mbali ya kuongoza EPL pia inaongoza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, huku Man City ikishika nafasi ya 22, imeshinda mechi mbili kati ya sita  na kutoa sare mbili.

Timu hii pia huenda ikapata ahueni mwakani na kiungo wao Rodri anatarajiwa kurudi baada ya kuanza kufanya mazoezi mepesi ili kujiweka fiti.

Kwa mujibu wa ripoti Rodri ambaye kwa sasa yuko nje baada ya kufanyiwa upasuaji anaweza akarejea uwanjani na kuitumikia Man City katika michuano ya Klabu bingwa dunia inayotarajiwa kupigwa Juni na Julai mwakani.

Fundi huyu ambaye aliumia Septemba mwaka huu katika mchezo dhidi ya Arsenal alidaiwa angekaa nje kwa muda mrefu zaidi lakini sasa maendeleo yake yanaonyesha kuwa atarejea mapema kuliko ilivyotarajiwa hapo awali.