James Milner wala hafikirii kutundika daruga
Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Liverpool na Manchester City, alianza kikosi cha kwanza kwa Brighton katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Brentford. Jumamosi. Huo ulikuwa mchezo wake wa 654 katika mashindano hayo ya Ligi Kuu England, akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na staa mwenzake wa zamani wa Man City, Gareth Barry.
LONDON, ENGLAND: KIRAKA James Milner ameashiria na bado hajapanga kustaafu soka baada ya kuvunja rekodi ya muda wote ya idadi ya mechi nyingi zaidi katika Ligi Kuu England.
Nyota huyo wa zamani wa Liverpool na Manchester City, alianza kikosi cha kwanza kwa Brighton katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Brentford. Jumamosi. Huo ulikuwa mchezo wake wa 654 katika mashindano hayo ya Ligi Kuu England, akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na staa mwenzake wa zamani wa Man City, Gareth Barry.
Sasa akiwa na umri wa miaka 40, Milner aliulizwa ni nini kimemwezesha kudumu kwa muda mrefu kiasi hicho na kujibu: “Ni ari na njaa ya mafanikio. Unataka kuwa bora kila siku iwe ni katika mechi au mazoezini. Nimezungukwa na vijana wengi, nataka kuchangia katika maendeleo ya taaluma zao, kuwachochea na kuwasaidia kufikia kiwango cha juu haraka iwezekanavyo.
“Hicho ndicho nilichokuja kufanya hapa. Nahisi bado ninaweza kuchangia dakika uwanjani. Nimekuwa na hali ya kukatishwa tamaa kidogo mwaka huu, labda kwa kutopata dakika nyingi, lakini ni uwiano mzuri kwa sababu tunapaswa pia kuendeleza wachezaji na tunataka kushinda.”
Milner anakabiliwa na uamuzi kuhusu mustakabali wake hivi karibuni. Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu, lakini inaonekana bado hafikirii kutundika daruga zake.
Aliongeza: “Natumaini nimeonyesha katika mechi chache zilizopita bado ninaweza kuchangia uwanjani. Nimefurahi kuwa sehemu ya kikosi hiki na chumba cha kubadilishia nguo, ambacho kimejaa wachezaji wenye tabia nzuri na vipaji vikubwa, pamoja na kocha mzuri anayekuja kwa kasi. Mambo hubadilika haraka katika soka. Unapokuwa na umri mkubwa, mambo yanaweza kubadilika kwa haraka zaidi. Kwa jeraha nililopata msimu uliopita sikuweza kuinua mguu wangu kwa miezi sita. Nitaendelea kujituma, tuone itatupeleka wapi.”
Milner alipokea pongezi nyingi kabla ya kuingia uwanjani kuitumikia Brighton. Mchezaji mwenzake wa zamani wa Liverpool, Jordan Henderson, alikuwa miongoni mwa waliompongeza, amesema: “Nilikuwa na bahati sana kuwa na Milly kama makamu wangu wa nahodha Liverpool, ingawa sikuwahi kumwona hivyo. Nilituona kama manahodha wawili. Alinisaidia sana, si tu uwanjani bali hata nje ya uwanja. Tulikuwa na uhusiano mzuri wa kikazi. Tulikuwa tunajiita ‘askari mwema na askari mkali’ nitawaachia ninyi mtambue nani alikuwa nani. Pia tulikuwa na urafiki mkubwa nje ya soka; wake zetu bado ni marafiki wa karibu na huwasiliana mara kwa mara.”
Milner alianza taaluma yake na Leeds United na baadaye akazichezea Newcastle United, Aston Villa, Man City na Liverpool Ligi Kuu England kabla ya kujiunga na Brighton mwaka 2023. Pia ameichezea timu ya taifa ya England mara 61.