Liverpool yaonywa kuhusu Robertson
Muktasari:
- Hatima ya beki huyo Mskochi ipo kwenye shaka kubwa huko Anfield kutokana na mkataba wake wa sasa kutarajia kufika tamati mwishoni mwa msimu.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imeonyesha kwamba itakuwa imepata hasara kubwa endapo kama itamruhusu beki wa kushoto Andrew Robertson aondoke katika klabu hiyo.
Hatima ya beki huyo Mskochi ipo kwenye shaka kubwa huko Anfield kutokana na mkataba wake wa sasa kutarajia kufika tamati mwishoni mwa msimu.
Kama Liverpool itachagua kutomsainisha beki huyo dili jipya, basi itamfanya mchezaji huyo kuondoka bure mwishoni mwa msimu wakati wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Robertson alisema wala hana presha juu ya hali yake ya sasa na amekubaliana na ukweli endapo kama huu utakuwa msimu wake wa mwisho kwenye klabu hiyo ya Anfield.
Lakini, staa wa zamani wa Liverpool, Jason McAteer alisema endapo kama timu hiyo itamruhusu beki huyo kuondoka basi itakuwa hasara kubwa kwao.
McAteer alisema: “Ni kitu kinachochekesha hakika Andy Robertson na Liverpool. Nadhani kwa muda ambao amekuwa akiichezea Liverpool, timu hiyo inapaswa kumpa nafasi nyingine. Sawa, wanaweza wasiwe na nguvu ya kumzuia akitaka kwenda Celtic.
“Naamini atapewa mkataba mpya, lakini utakuwa na masharti tofauti. Liverpool ipo kwenye kipindi kama kilichoikabili Man City msimu uliopita, timu yao imechoka. Jurgen Klopp ameichosha timu.
Kuna wachezaji kadhaa wameondoka kwenye kikosi hicho akiwamo James Milner na Jordan Henderson pamoja na Adam Lallana waliokuwa viongozi kwenye timu, hivyo kikosi kwa sasa kimebaki na wachezaji kama Andy Robertson, ambao wanapaswa kuendelea kupewa nafasi ya kubaki kwenye kikosi hicho cha Anfield.
Robertson, 31, alisajiliwa na Liverpool akitokea Hull City mwaka 2017. Amecheza mechi 354 kwenye kikosi hicho na kuisaidia Liverpool kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA na Kombe la Ligi mara mbili.