James Harden akamatwa Houston
Muktasari:
- Kwa mujibu wa rekodi za mahakama zilizoripotiwa na Houston Chronicle, Harden alikuwa akiendesha gari aina ya Mercedes katikati mwa jiji la Houston majira ya saa 3:40 asubuhi alipokuwa amesimama nyuma ya gari jingine ambalo lilikuwa limesimamishwa na polisi karibu na eneo la 1600 Jefferson.
NEW YORK, MAREKANI: NYOTA wa NBA, James Harden ameanza kipindi cha mapumziko ya msimu akiwa na changamoto mpya nje ya uwanja baada ya kukamatwa mapema Jumamosi mjini Houston na kushtakiwa kwa kosa la kubeba silaha kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa rekodi za mahakama zilizoripotiwa na Houston Chronicle, Harden alikuwa akiendesha gari aina ya Mercedes katikati mwa jiji la Houston majira ya saa 3:40 asubuhi alipokuwa amesimama nyuma ya gari jingine ambalo lilikuwa limesimamishwa na polisi karibu na eneo la 1600 Jefferson.
Wakati wa mahojiano hayo, polisi wanadaiwa kuona bastola ndani ya kishikio cha vikombe kwenye gari la Harden.
Rekodi za mahakama zinaeleza kuwa Harden aliwaambia polisi kwamba silaha hiyo ilikuwa yake. Baada ya hapo alikamatwa na kupelekwa katika gereza la Harris County kabla ya kuachiwa kwa dhamana baadaye siku hiyo.
Tuhuma Zinazomkabili
Malalamiko yaliyotajwa katika ripoti mbalimbali yanamshutumu Harden kwa: Kumiliki bastola ndani ya gari "kwa makusudi na kwa ufahamu wake" kinyume na sheria.
Ripoti nyingine zinaeleza kuwa silaha hiyo ilikuwa wazi kuonekana ndani ya gari na haikuwa imehifadhiwa katika kifaa maalumu cha kubebea silaha.
Harden anatakiwa kufika mahakamani tena tarehe 22 Juni kwa ajili ya kusomewa rasmi mashtaka.
Hadi wakati taarifa hizi zilipotolewa, Harden alikuwa hajatoa kauli yoyote hadharani kuhusu tukio hilo, na wawakilishi wake pia hawakuwa wametoa taarifa rasmi.
Masharti ya Dhamana
Ingawa kosa analokabiliwa nalo ni la kiwango cha chini , masharti ya dhamana yake yanaweka vikwazo kadhaa wakati kesi ikiendelea.
Kwa mujibu wa TMZ, Harden amekatazwa:
Kumiliki au kubeba silaha yoyote. Kumiliki risasi au vifaa vingine vya kijeshi. Kutumia au kumiliki pombe.
Kutumia dawa za kulevya au bangi isipokuwa kama ameandikiwa na daktari. Kutumia dawa hatari zisizoidhinishwa.
Pia anatakiwa kukubali kufanyiwa vipimo vya mkojo vya kushtukiza ili kuthibitisha kuwa anazingatia masharti hayo.
Athari kwa Kipindi cha Mapumziko
Kukamatwa kwa Harden kunakuja wakati ambapo tayari kulikuwa na maswali mengi kuhusu mustakabali wake wa kikapu na mipango yake kwa msimu ujao wa NBA.
Kwa sasa, kesi hiyo itafuatiliwa kwa karibu huku mashabiki na wadau wa NBA wakisubiri kuona hatua zitakazofuata kutoka kwa mahakama na kutoka kwa Harden mwenyewe