Isak, Newcastle hakuna matata
Muktasari:
- Isak alilazimisha uhamisho wa kuachana na Newcastle kwenye dirisha la majira ya kiangazi na alifanikisha mpango wake huo kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili alipojiunga na Liverpool kwa ada iliyovunja rekodi ya uhamisho Uingereza.
NEWCASTLE, ENGLAND: STRAIKA, Alexander Isak meseji yake ya mwisho kwenye grupu la WhatsApp la wachezaji wa Newcastle United ilikuwa kuwashukuru kwa kumbukumbu zote walizofanya pamoja huku Dan Burn akimjibu "kiroho safi, hakuna uadui."
Isak alilazimisha uhamisho wa kuachana na Newcastle kwenye dirisha la majira ya kiangazi na alifanikisha mpango wake huo kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili alipojiunga na Liverpool kwa ada iliyovunja rekodi ya uhamisho Uingereza.
Isak hakucheza mechi yoyote kati ya tatu za kwanza ilizocheza Newcastle kwenye Ligi Kuu England na alikuwa akifanya mazoezi kivyake.
Jambo hilo lilimfanya Isak kukosolewa sana kwa kulazimisha uhamisho na kuaminika kwamba hilo lingemfanya kutibuana na wachezaji wenzake.
Wachezaji wa Newcastle walikumbana sana na maswali ya sakata hilo la Isak kila walipokutana na waandishi wa habari kwamba atabaki St James' Park au la. Burn alisema kama klabu itapata dili nzuri basi litamalizwa vizuri kwa pande zote mbili na ndicho kilichokwenda kutokea.
Burn alisema: "Alex ni mchezaji mwenzangu, hivyo hii ilikuwa ngumu sana, lakini nimefurahi mwisho umekuwa mzuri kwa mchezaji, amepata kile alichokuwa akikitaka.
"Alituma meseji kwamba anaondoka, anashukuru kwa kumbukumbu nzuri na vitu vingine na wachezaji wote, walimjibu vizuri. Lakini, nilichosema, nadhani Alex amepata alichokuwa akikitaka na sasa tunawekeza akili zetu kwenye kila tunachoweza kukifanya. Jambo lake lilitugusa kidogo, lakini hakuna uadui."
Burn na Isak ndio waliofunga mabao kwenye fainali ya Kombe la Ligi msimu uliopita wakati Newcastle ilipoichapa Liverpool na kunyakua taji lao la kwanza baada ya miaka 70. Kuondoka kwa Isak kumeifanya Newcastle United kuwa na nafasi ya kuwasajili Nick Woltemade na Yoane Wissa kuboresha safu ya ushambuliaji ambapo wataungana na Anthony Elanga.
USAJILI GHALI
UINGEREZA!
1.Alexander Isak, Pauni 130milioni
2.Florian Wirtz, Pauni 116.5milioni
3.Moises Caicedo, Pauni 115milioni
4.Enzo Fernandez, Pauni 106milioni
5.Declan Rice, Pauni 105milioni
6.Jack Grealish, Pauni 100milioni
7.Romelu Lukaku, Pauni 97.5milioni
8.Paul Pogba, Pauni 89milioni
9.Antony, Pauni 85.5milioni
10.Harry Maguire, Pauni 85milioni